2018-06-02 09:35:00

Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani na Fumbo zima la Wokovu!


Utangulizi: Mwokozi wetu, Katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, Karamu ya Pasaka ‘ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele’. Sherehe ya Ekaristi Takatifu tunayoiadhimisha leo tunasherehekea uwepo hai wa Bwana Wetu Yesu Kristo katika Mwili na Damu yake azizi chini ya maumbo ya mkate na divai na tunamwomba Mungu ili sisi tunaoshiriki mafumbo haya matakatifu tuyatafsiri katika maisha yetu hapa duniani na yatustahilishe kuufikia uzima wa milele.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Kut. 24:3-8) linaeleza namna ambavyo Mungu alifunga agano na watu wake Israeli chini ya mtumishi wake Musa. Hili ndilo hasa Agano la Kale. Kwanza Musa aliwaelezea waisraeli maneno yote ya Bwana, nao waliyasikiliza na wakakubali wakisema “maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda”. Kuweka agano lenyewe Musa alijenga altare, akaweka nguzo 12 kuwakilisha makabila 12 ya Waisraeli na kisha akachinja sadaka ya kuteketeza na sadaka ya amani. Nusu ya damu ya mnyama akanyunyiza altareni, ndio kuonesha kuwa Waisraeli sasa wanajitoa kikamilifu kwa ajili ya Bwana, watamtii na kumpa utukufu anaostahili. Sehemu ya damu iliyobaki ambayo sasa tayari Bwana ameshaipokea akawanyunyizia watu, ndio alama ya kuomba na kupokea baraka kutoka kwa Bwana kwa Agano hilo wanaloliweka.

Agano hili la kale ndilo ishara ya Agano Jipya atakaloliweka Kristo kwa Damu yake na ndiyo ishara ya mwendelezo wa sadaka hiyo ya Agano Jipya katika adhimisho la Ekaristi Takatifu. Kama katika Agano la Kale watu walivyosikiliza maneno ya Bwana ndivyo hata leo adhimisho la Ekaristi huanza kwa kusikiliza Neno la Bwana. Nasi huitikia “Amina” ndiyo kukiri kuwa “Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda”. Baada ya kusikiliza Neno, Altare huandaliwa na sadaka ile ile ya Kristo Msalabani hutolewa, sadaka ambayo waamini huishiriki na huipokea.

Somo la Pili (Ebr. 9:11-15) linaelezea ukuu wa sadaka ya Kristo. Kisha kuweka Agano wakati wa Musa, Waisraeli waliendelea kujitakasa mbele ya Bwana  na waliendelea kupyaisha Agano hilo kwa njia ya sadaka mbalimbali. Kuu ilikuwa ni ile aliyoitoa kuhani mara moja kila mwaka akiingia patakatifu pa patakatifu. Somo hili linalinganisha sadaka hizi na ile aliyoitoa Kristo Msalabani. Linaonesha kwanza kuwa Kristo ndiye kuhani mkuu halisi na yeye haingii patakatifu pa patakatifu palipoandaliwa kwa mikono ya binadamu bali anaingia mbinguni. Tena yeye hana haja ya kutoa sadaka mara kwa mara bali alitoa mara moja tu na ikatosha kwa enzi zote. Hali kadhalika sadaka aliyoitoa Kristo ina thamani kubwa kuliko ile iliyotolewa katika Agano la Kale kwa sababu ile ya Agano la Kale ilikuwa ni ya wanyama ilhali hii ni ya Mwana wa Mungu.

Kufafanua hili Mtakatifu Yohane Krisostom anasema wanyama waliokuwa wanatolewa katika Agano la Kale hawakuwa na utashi, walikuwa wanalazimishwa bali Kristo anajitoa mwenyewe kwa uhuru na utashi kamili. Somo linaongeza pia kuwa sadaka ile ya Agano la Kale haikuwa na uwezo wa kuondoa dhambi. Ilikuwa ni kama kusafisha mwili kwa nje, bali sadaka ya Agano Jipya inaondoa dhambi na kuutakasa mwili na uovu wote. Hii ndiyo sadaka ya Kristo, sadaka ya Agano Jipya; ndiyo Ekaristia.

Injili (Mk. 14:12-16, 22-26) inaelezea tukio la kuwekwa kwa Ekaristi. Kristo anakula Pasaka pamoja na wanafunzi wake. Ni katika chumba cha juu, katika orofa kubwa ambapo Kristo anawalelekeza wanafunzi wake kuandaa karamu hiyo. Hapa tayari tunaona utofauti fulani. Karibu mara zote Krito amekula na wanafunzi wake hata na wafuasi wengine katika maeneo ya kawaida; chini, uwandani au katika miji ya familia za watu ila hapa anachukua chumba maalum na kilichofanyiwa maandalizi maalum. Hii inadokeza kuwa kile kinachoenda kufanyika huko pia kinavuka ile hali ya kawaida na kina umaalumu wake.

Walipokuwa wakila ndipo Kristo akaweka Ekaristi. Akatwaa mkate akaubariki, akashukuru na akawaambia “Twaeni mle nyote huu ndio Mwili wangu” na kisha kwa divai “twaeni mnywe nyote hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili ya wengi”. Ukamilifu wa Agano hili jipya ulitokea pale Msalabani alipoutoa kweli Mwili wake na alipomwaga kweli Damu yake azizi kuanzisha Agano Jipya na la milele kwa ajili ya maondoleo ya dhambi.

Tafakari: Kuhusu Ekaristi, Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa Ekaristi ndiyo jumla na muhtasari wa imani yetu nzima (KKK 1327). Imani yetu na fumbo zima la wokovu wa mwanadamu vimelala juu ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo ishara thabiti ya ushirika katika uzima wa kimungu na adhimisho lake ni ishara ya muunganiko na liturujia ya mbinguni. Ekaristi ndio chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Kumbukumbu rasmi ya kuwekwa kwa Ekaristi ni siku ya Alhamisi Kuu. Lakini kama tunavyofahamu ilivyo nidhamu ya maadhimisho ya Juma Kuu hasa zile siku tatu kuu za Pasaka, hatuwezi kuadhimisha siku hiyo kwa shangwe kuu pamoja na maandamano ya kutangaza ukuu wa fumbo hili ambalo Kristo ameliachia Kanisa. Ndiyo maana ikatengwa siku hii baada ya sherehe za Pasaka kwa ajili ya adhimisho hili kubwa la Ekaristi.

Katika kulitafakari Fumbo hili la Ekaristi, leo nawaalika tuyatafakari maneno haya “akashukuru, akaumega na akawapa”. Haya ni maneno ambayo huwa tunayasikia kila inapoadhimishwa Ekaristi Takatifu. Padre mwadhimishaji katika mageuzo ya mkate kuwa mwili wa Yesu husema “akashukuru, akaumega na akawapa wafuasi wake akisema.. twaeni mle nyote...” (Rej. Sala ya Ekaristi ya III).

Neno akashukuru hueleza maana halisi ya neno Ekaristi. Ekaristi maana yake ni shukrani. Ni sadaka ya shukrani kwa Baba na ni baraka ambayo kwa njia yake Kanisa huonesha shukrani yake kwa Mungu kwa ajili ya fadhili zake zote. Tunapoishiriki Ekaristi, nasi tunaalikwa kuwa watu wa shukrani. Kuwa na shukrani kwa Mungu kwa yote na kumshukuru yeye daima katika kila hatua na kama anavyotukumbusha Mt. Paulo, kushukru kwa kila jambo. Tunaalikwa pia kuwa na shukrani kwa watu kwa fadhili mbalimbali wanazotutendea. Kushukuru ni kuthamini, kushukuru ni kutambua, kushukuru ni kukumbuka, kushukuru ni kuomba tena.

Neno akaumega linadokeza umoja wa Mwili wa Fumbo ambao wote unashiriki mkate mmoja unaomegwa na wote wanaoshiriki wanaunganishwa kuwa mwili mmoja. Na hiyo pia ndiyo sala ya Kanisa ili wote wanaoshiriki mwili huo na kukinywea kikombe hicho Roho Mtakatifu awaunganishe ili wawe mwili mmoja na roho moja katika Kristo. Kumbe kushiriki Ekaristi na hapo hapo kuendeleza utengano au mgawanyiko wa aina yoyote ni kasoro na mapungufu makubwa. Kama vile kushiriki pamoja meza ya chakula kulivyo alama ya mapatatano, kushiriki meza ya Ekaristi kunapaswa kuwa alama zaidi ya upatano na umoja katika familia, katika jumuiya na katika Kanisa zima. Upatano kati ya mapadre wanaoadhimisha pamoja Ekaristi, upatano kati ya wanafamilia wanaopokea Ekaristi, upatano kati ya Wanajumuiya (Jumuiya za kitawa, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo) na upatano kwa waamini wote.

Neno akawapa ni neno linaloalika upendo kwa wote wanaoshiriki Ekaristi. Upendo wa kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Ekaristi yenyewe ni sadaka. Ni sadaka ya Mwili wake alioutoa Yesu na Damu yake azizi aliyoimwaga kwa ajili ya fidia ya wengi. Yeye mwenyewe alisema “hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ndivyo tunavyoalikwa kuuiga upendo huu kila tunaposhiriki Ekaristi. Kutoka nje yetu na kutenda yaliyo zaidi ya maslahi yetu, kumpa sikio anayehitaji kusikilizwa, kumpa muda anayehitaji ukaribu wetu, kurudisha furaha kwa wanaoikosa na kitulizo kwa wanaosumbuka. Upendo wa kujiachia kwa ajili ya mafaa ya wengine na zaidi kwa ajili ya wokovu wao. Amina.

Padre William Bahitwa.

Vatican News.

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.