2018-06-02 14:00:00

Askofu Sangu: Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo!


Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hii ni zawadi ya upendo inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwa namna ya pekee kabisa linamwonesha Yesu kuwa kweli ni mwanakondoo wa Mungu na sadaka inayotolewa kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele!

Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha Kristo anayejitoa mwenyewe kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa pamoja na utendaji wake. Hii ni Sakramenti ya umoja wa Kanisa, inayoimarisha na kudumisha upatanisho kati ya Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anakaza kusema, Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kuadhimishwa kwa Ibada, Uchaji wa Mungu na Uaminifu, ili kuonja: uzuri, ukuu na utakatifu wa Sakramenti hii ya ajabu inayoonesha Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu.

Hiki ni kielelezo cha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kwa hulka yake Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya amani inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, ndiyo maana Mama Kanisa anawahamasisha waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa na ushiriki hai katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Waamini wajitahidi kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa uchaji na ibada, ili Fumbo hili liweze kuwa ni chachu ya kupyaisha maisha, wito na utume wao sehemu mbali mbali za dunia kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Hii ni chachu ya maadili na utu wema; inayowahamasisha waamini kutoka katika ubinafsi wao, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania anakiri kwamba, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni amana, utajiri na urithi wake wa maisha ya kiroho, kwani Ekaristi Takatifu ni chimbuko na kilele cha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Huu ndio ule upendo wa Kimungu ambao Askofu Sangu anataka kuumwilisha katika maisha na utume wake kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Shinyanga, ili kukuza na kudumisha: utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu. Muhtasari wa upendo unadadavuliwa kwa kina na mapana na Mtume Paulo katika utenzi wa upendo kwenye Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho Sura ya 13: 1-13. Lengo ni kuimarisha Injili ya upendo na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Shinyanga. Askofu Liberatus Sangu anakaza kusema, penye upendo pana umoja, mshikamano na amani. Bila upendo yote ni ubatili mtupu! Kila mtu anapaswa kutendwa wema kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, lengo kuu ni kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.