2018-06-02 14:00:00

Askofu mkuu Kivuva Musonde: Ekaristi ni Sakramenti ya haki na amani


Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, kila mwaka, Mama Kanisa anawapatia watoto wake fursa ya kutangaza, kushuhudia, kuabudu na kuitukuza Sakramenti kuu kwa maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu: Sadaka takatifu iliyotolewa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Katika sherehe ya Ekaristi Takatifu, Kanisa linashangilia na kukiri kwa jicho la imani, uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja nao kwa njia ya maumbo ya Mkate na Divai; Mwili na Damu yake Azizi.

Askofu mkuu Musonde anasema, huu ni muhtasari wa imani, maisha na utume wa Kanisa unaowasukuma waamini kuwaona jirani zao kama “Sakramenti na zawadi ya pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu” ili kuwaonjesha upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Kwa njia hii, waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu ambao ni wa milele na wa ulimwengu wote; ufalme wa kweli na wa uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani.

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anakaza kusema, Sherehe ya Ekaristi Takatifu, iwe ni fursa kwa waamini kuweza kuiadhimisha, kwa Ibada, Uchaji, Uelewa na Ushiriki mpana zaidi, ili hatimaye, waweze: Kumwabudu, kumsujudia na kumwamini Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao. Maadhimisho haya ni uthibitisho wa jicho la imani juu ya uwepo hai wa Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi! Ekaristi Takatifu ni kanuni na mpango wa maisha ya Kanisa katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya, ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki, amani, umoja na udugu! Ekaristi Takatifu ni chachu ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.