2018-06-01 08:36:00

FUMBO LA EKARISTI TAKATIFU: Yesu: Kuhani, Altare na Sadaka!


Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ni Sakramenti iliyowekwa na Kristo mwenyewe kuwa ishara ya uwepo wake endelevu na muunganiko kati yake na sisi. Katika Sakramenti hii tunampokea Kristo mzima katika maumbo ya mkate na divai. Kwa njia hiyo tunafanywa kuungana na nafsi yake na hivyo kuunganishwa na umungu. Ubinadamu na umungu vinaungana kwa namna dhahiri kabisa. Yeye anayeishiriki Sakramenti hii kama asemavyo Mtakatifu Augostino “anafanyika kile anachokipokea”. Kwa kuwa katika Ekaristi Takatifu kuna uwepo halisi wa Kristo basi sisi tunaoshiriki chakula hivi tunafanyika kuwa Kristo na hivyo kushiriki katika Agano Jipya.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatuambia hivi: “Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili na Damu yake azizi. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, Ukumbusho wa kifo na ufufuko wake: Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele” (Namba 1323). Hivyo kwanza kabisa Ekaristi Takatifu ni karamu ya Pasaka. Masomo yetu ya leo yanairandanisha sadaka ya Ekaristi Takatifu na Pasaka ya Wayahudi huku tukielekezwa kuuona ukuu wa sadaka ya Kristo ambayo pia hiutwa sadaka ya Agano jipya na la milele.

Somo la kwanza linaonesha jinsi ambavyo tangu zamani Wayahudi walivyoweka Agano na Mungu kwamba watalifuata Neno lake na kutii amri na maagizo yake kwa sadaka ya Damu. Sadaka ilikuwa ni ishara ya utii kwa Mungu: “Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii”. Ni ishara ya kulipokea Neno lake na kufuata maagizo yake. Sadaka ya damu iliwaunganisha Wayahudi na Mungu. Madhehebu ya sadaka hiyo yalimwonesha Musa akipanda mlimani pamoja na baadhi ya wazee wa Israeli ili kutolea sadaka ya Agano. Musa alijenga Altare inamwakilisha Mungu. Kitendo cha kunyunyuzia damu altare na kisha damu hiyo kunyunyuziwa watu wote kiliwaunganisha watu wote na Mungu na kufanya Agano.

Somo la pili linatuinua katika sadaka iliyo kuu zaidi. Hii ni sadaka ya Kristo ambayo inautanabaisha ukuu wake katika namna zifuatazo. Kwanza Kristo mwenyewe anajitambulisha kama Kuhani mkuu; Ni Yeye ambaye anaiadhimisha sadaka hiyo. Ukuu wake unatokana na haiba yake. Yeye aliye Mungu kweli na mtu kweli anakuwa kwetu kama “mjumbe wa Agano jipya”. Pili ukuu huo unajionesha katika mahali inapoadhimishiwa. Ni katika “hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake isiyo ya ulimwengu huu”. Tatu Yeye mwenyewe ni Sadaka. Damu inayotolewa kwa sadaka hii “si damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe”. Sadaka hii imefanyika mara moja na ni ya milele. Sadaka hii ilitakasa roho na kuleta wokovu. Kristo, “kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa. Itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai”.

Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anatukumbusha juu ya sadaka za wanyama ambazo ziliwatakasa Wayahudi kwa nje tu: “damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama na ya ng’ombe waliyonyunyuziwa wenye uchafu hutakasa hata kusafisha mwili”. Anaendelea kutuambia kuwa sadaka ya Kristo ni kuu zaidi kwani huwatakasa waamini na kuwafanya watakatifu. Hii ni kwa sababu sadaka yake inaadhimishwa katika hema yenye asili yake mbinguni na siyo kwa wanadamu. Ukombozi wa mwanadamu unawezekana tu pale asili yake au chanzo chake kinapoanzia kutoka juu. Hii inatufunulia namna ambavyo dhambi ilivyoiharibu haiba ya ubinadamu na kumfanya asiweze kujinasua kwenye shimo la dhambi. Hivyo sadaka ya Kristo kwa namna nyingine inatufunulia upendo wa Mungu anayekubali kushuka na kuja tena kuwatafuta watu wake.

Sadaka hii ya Kristo ambayo aliitoa pale juu msalabani inafumbatwa katika fumbo la Ekaristi Takatifu. Kila siku jamii ya waamini inapoadhimisha sadaka ya Ekaristi Takatifu inaendelea kuweka hai sadaka ya Kristo Msalabani. Ekaristi Takatifu ni “Sadaka takatifu kwa sababu yaifanya iwepo sadaka ile moja ya Kristo Mwokozi inayojumlisha matoleo ya Kanisa. Sadaka takatifu ya Misa, sadaka ya masifu, sadaka ya roho, sadaka safi na takatifu, kwani inakamilisha na kupita sadaka zote za Agano la Kale” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Namba 1330).

Wakati wa Karamu ya mwisho kama ifafanuavyo Injili ya leo, Kristo alionesha mabadiliko hayo, yaani kutoka sadaka ya kale kwenda sadaka mpya aliyoiadhimisha katika mwili wake: “Alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akwawapa akisema, Twaeni; huu ndiyo mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa wakakinywea wote. Akawambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi”. Karamu ya Pasaka ya kale ya Wayahudi iliadhimishwa kwa sadaka ya damu ya mbuzi au kondoo na mikate isiyotiwa chachu. Kristo alipokuwa akiiadhimisha pamoja na wanafunzi wake aliibadilisha maana yake na kujitoa yeye kama mkate na damu yake kuwa ni ya agano jipya kati ya Mungu na watu wake. Sadaka hii ni Ekaristi Takatifu.

Kumbe, Ekaristi Takatifu ni Sadaka ya Agano jipya kati ya wanadamu na Mungu. Ni sadaka inayotutakasa na kutufanya kuwa watakatifu mbele za Mungu. Ni sadaka inayotuunganisha na Mungu. Tuijongeapo karamu hii hatuna budi kujihoji na kujiweka tayari kulishika agano hilo katika maisha yetu. Yeye anayeshiriki chakula hiki anaanzisha uhusiano na Mungu. Uhusiano huo na Mungu unajidhihirisha katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku. Mwili na damu ya Kristo ni ishara za uwepo Mungu kiuhalisia katika maisha ya kila mmoja anayepokea. Kristo anamwilika na kuishi katika kila nafsi ya mmoja wetu. Hapa ndipo tunapata changamoto katika maisha yetu ya kila siku.

Changamoto kubwa inajitokeza katika maisha yetu baina ya wana Kanisa. Kwa bahati mbaya sana wengi wetu tumekuwa watu wa kujikinai utakatifu na kujithibitisha mbele za watu kwa kushiriki Ekaristi Takatifu. Wakati mwingine tunakuwa mahakimu na maaskari kanzu kwa kuwazuia na kuwafungia wengine kushiriki karamu hii ya kimbingu. Tutakapojiweka katika hali hiyo na kushindwa kuzisafisha dhamiri zetu kwa matendo mema toka ndani ya mioyo yetu hakika tunajidanganya wenyewe. Agano tunalolifanya kwa njia ya chakula hiki ni kati yako wewe na Mungu. Yeye hadanganyiki na anaona hadi ndani ya moyo wako.

Tuepuke kukifanya chakula hiki kama maonesho na ‘kujishebedua’ utakatifu wetu. Sadaka hii ya Agano jipya itupatie changamoto daima kuona namna tunavyotimiza nyajibu zetu mbalimbali kadiri ya Agano hilo. Tutimize vema nyajibu hizo kusudi kubaki waamifu kwa agano letu na Mungu na pale tunapokengeuka tumjongee kwa moyo wa toba na kuomba msamaha kwa maana Upendo wake mkuu wadumu milele.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.