2018-05-31 07:57:00

Maandamano ya Ekaristi Takatifu: Uwepo endelevu wa Kristo!


Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila Mwaka Mama Kanisa anayofuraha kubwa ya kusherehekea na kushuhudia Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kwa maandamano makubwa, ushuhuda kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuandamana na waja wake katika historia ya maisha yao ya kila siku hadi utimilifu wa dahali.

Askofu msaidizi Paolo Lojudice wa Jimbo kuu la Roma anasema, mwaka huu, Baba Mtakatifu Francisko anarejesha tena utamaduni na Mapokeo yaliyoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI hadi kufikia mwaka 1978 kwa kutembelea na kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu katika maeneo mbali mbali ya Jimbo kuu la Roma. Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea eneo la Ostia! Kwa wakristo wanaoamini, maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu ni ushuhuda kwamba, kwa mara nyingine tena, Kristo Yesu anawatembelea waja wake katika hali na mazingira yao; tayari kujikita katika furaha ya Injili na upendo katika maisha yao.

Askofu msaidizi Paolo Lojudice  anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, hii ni changamoto ya kuondokana na umaskini mkubwa wa maadili na utu wema, ili kuibua tena imani na matumaini, kwa kutambua uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yao. Maandamano haya ni fursa ya kubomolea mbali kuta za utengano: kiroho, kimwili na kisaikolojia, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa familia ya Mungu katika utofauti na utajiri wake. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha Injili ya familia na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kijamii!

Don Carmelo Di Giovanni Paroko wa Parokia ya “Regina Pacis”, huko Ostia, Jimbo kuu la Roma anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu anapenda kutoa mwaliko kwa waamini kusimama tena katika imani, matumaini na mapendo na kuendelea na safari ya maisha yao ya kiroho. Watambue kwamba, Maandamano makubwa ya Ekaristi ni kielelezo cha Kristo Yesu anayetaka kuwarejeshea waja wake matumaini katika maisha, kwani hawa ni watu ambao wamejeruhiwa vibaya kutokana na umaskini wa hali na kipato pamoja na hali ngumu ya maisha. Yesu anataka kutembea na kuandamana na waja wake waliojeruhiwa kiroho na kimwili; wenye shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha, lakini wenye matumaini ya kuweza kuanza tena upya, hija ya maisha yao ya kiroho.

Ni changamoto kwa wakleri na viongozi wa Kanisa kujenga na kudumisha moyo wa huduma makini kwa familia ya Mungu, daima wakithubutu kutoka nje ya Sakristia na kuwaacha wale kondoo 99, ili kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea njia, ili naye, aweze kuonja tena huruma na upendo wa Baba wa milele kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa muda wa miaka 40, Don Carmelo Di Giovanni anasema, amekuwa akitoa huduma kwa wafungwa magerezani huko London, nchini Uingereza, yaani kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 2014 na kuamua kurejea tena huko Ostia nje kidogo ya Roma. Katika maisha na utume wake, ameonja na kuona cheche ya toba na wongofu wa ndani kutoka kwa wafungwa; waliojipatanisha na Mungu kwa njia ya Kanisa, baada ya kuogelea katika dimbwi la dhambi na mauti; magonjwa na hali ya kujikatia tamaa, wakabahatika kukutana na Kristo Yesu katika njia ya maisha yao.

Don Carmelo Di Giovanni anaendelea kusema kwamba, watu wana kiu ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; wanataka kusikiliza Neno la Mungu linalomwilishwa kwenye matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Maandamano ya Ekaristi Takatifu kwa mwaka huu wa 2018, iwe ni fursa kwa waamini: kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kumruhusu Kristo Yesu kutembelea na kuganga maisha yao! Hivi karibuni, eneo la Ostia limekumbwa na kashfa ya vitendo vya kigaidi vinavyochafua utu na heshima ya binadamu.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amechambua kwa kina mapana magonjwa ya maisha ya kiroho na tiba yake, ili kuweza kupyaisha maisha na utume wa Kanisa; kwa kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya kiroho; kwa kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikilizana katika ukweli na uwazi pamoja na kuendelea kujikita katika maisha na utume wa Kanisa ambalo kimsingi ni Mama na Mwalimu.

Ekaristi Takatifu ni kiini cha imani ya Kanisa. Waamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili, tarehe 3 Juni 2018 wataadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Sherehe hii kwenye Parokia ya Mtakatifu Monica, huko Ostia, nje kidogo ya mji wa Roma. Baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu ataongoza maandamano ya Ekaristi Takatifu na kuhitimishwa kwenye Parokia ya “Nostra Signora di Bonaria” na baadaye atatoa baraka ya Ekaristi Takatifu.

Kila Jumapili, Siku ya Bwana, waamini wanaadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, Siku ile ya Alhamisi kuu wakati wa Karamu ya Mwisho! Lakini, kila mwaka, Kanisa lina furaha kubwa ya kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, kiini cha imani ya Kanisa kwa kumwabudu Kristo Yesu anayejisadaka na kujitoa kwa waja wake kama chakula na kinywaji cha wokovu! Kristo Yesu ni mkate na kinywaji kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele; ni sadaka ya Kristo mwenyewe kwa ajili ya binadamu! Mwana wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu ni Mwana Kondoo wa Pasaka, anayemkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa lindi la dhambi na mauti na kumwongoza katika Nchi ya ahadi.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili  kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ni uwepo endelevu wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya waamini mahali popote pale walipo: mjini na vijijini; Kaskazini na Kusini mwa dunia; katika nchi ambazo kimsingi zina utamaduni na Mapokeo ya Kikristo na hata katika Nchi zile ambazo zimeinjilishwa hivi karibuni. Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Yesu anajisadaka mwenyewe kama nguvu ya maisha ya kiroho ili kuwajengea uwezo wafuasi wake wa kumwilisha Amri ya upendo: kwa kupenda kama alivyopenda Yeye mwenyewe; kwa kujenga na kudumisha jumuiya inayomsimikwa katika ukarimu, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kulishwa na Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kujiaminisha kwake na kumwachia nafasi ili aweze kuwaongoza. Huu ni mwaliko wa kumpokea na kumpatia Kristo Yesu nafasi ya kwanza katika maisha, tayari kupokea na kumwilisha upendo unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, dhamana ya Roho Mtakatifu anayerutubisha na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani; watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao!

Kwa kulishwa na kunyweshwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, waamini wanakuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kuhamasishwa kujenga na kudumisha umoja na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kama ambavyo waamini wanavyokumbushwa na Mtakatifu Paulo, Mtume! Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo na umoja. Hii ni kumbu kumbu yenye uvumilivu kwani hata katika magumu ya maisha, bado waamini wanatambua kwamba, Roho wa Kristo yuko ndani mwao.

Ekaristi Takatifu inawatia shime kusonga mbele kwani hata katika safari ambayo ni ngumu kiasi gani, waamini wanatambua kwamba, hawako pweke, na kamwe Kristo Yesu hawezi kuwageuzia kisogo na kwamba, kila wakati wanapomwendea anawapatia nguvu mpya kwa njia ya upendo wake. Ekaristi Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, hawapo peke peke, bali ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; familia ya Mungu kama ilivyojionesha kwenye Agano la Kale ilipokusanyika kwa ajili kuokota manna iliyoshuka kutoka mbinguni.

Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, anawaalika waamini kumpokea kwa pamoja na kumshikiri kati yao. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbu kumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.