2018-05-30 09:41:00

Changamoto za maisha na utume wa Kanisa Katoliki Burkina Faso-Niger


Hija za kitume zinazofanywa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican ni nafasi kwa viongozi wa Makanisa mahalia kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake kuhusu maisha na utume wa Makanisa mahalia. Ni fursa ya kusali, kutafakari kuhusu matatizo, changamoto na fursa za Makanisa mahalia katika mchakato mzima wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji! Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger, limehitimisha hija yake ya kitume mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, 28 Mei 2018.

Burkina Farso na Niger ni nchi ambazo zina idadi kubwa zaidi ya waamini wa dini ya Kiislam. Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso-Niger linaongozwa na Askofu mkuu Paul Yembuado Ouedraogo na lina majimbo makuu matatu yanayoundwa na majimbo 12 na Kanisa Katoliki nchini Niger lina majimbo mawili tu! Kumbu kumbu za kihistoria zinaonesha kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Burkina Faso kunako mwaka 1980 na kurejea tena huko mwaka 1990. Burkina Faso ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican kunako mwaka 1973.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso, kunako mwaka 2010 likafanya hija ya kitume mjini Vatican na kubahatika kukutana na Papa Mstaafu Benedikto XVI aliyepongeza uhusiano na mafungamano mazuri kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo nchini humo; ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa familia ya Mungu nchini Burkina Faso. Mwaka 2016 Baba Mtakatifu Francisko akakutana na Rais Roch Marc Christian Kaborè.

Viongozi hawa wawili wakakazia tena umuhimu wa upatanisho wa kitaifa, umoja, ushirikiano na mshikamano kati ya waamini wa dini mbali mbali nchini humo; umuhimu wa kuibua mbinu mkakati utakaowawezesha vijana kupata fursa za ajira pamoja na kupongeza mchango wa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya watu wa Mungu nchini Burkina Faso. Maaskofu wanasema, kwa sasa changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambayo imekuwa ni chanzo kikubwa cha mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Al Qaeda.

Waamini wa dini mbali mbali watambue na kuthamini tofauti zao kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si sababu ya kupelekea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini. Umoja wa kitaifa ni jambo muhimu sana kwa ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Viongozi wa Serikali wanapaswa kuheshimu Katiba ya nchi; Uhuru wa kuabudu pamoja na kudumisha haki msingi za binadamu. Kanisa wakati wote, limeendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, kwa kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili na utamaduni wa amani na upatanisho wa kitaifa.

Changamoto ya pili ni mapambano dhidi ya baa la njaa,utapiamlo wa kutisha, umaskini na ujinga; ili kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na kuendeleza maboresho katika sekta ya elimu, afya na huduma za jamii. Kanisa pia linaendelea kujizatiti katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Lengo ni kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki, amani na udugu wa kweli.

Changamoto ya tatu ambayo ni kubwa kwa Kanisa Katoliki nchini Niger ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wanaohudumiwa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kutoka ndani na nje ya Niger bila kuwasahau waathirika wa vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram kutoka Nigeria. Kanisa nchini Burkina Faso limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama njia ya kudhibiti kuenea kwa Jangwa pamoja na athari za mabadiliko makubwa ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza wananchi katika maafa na majanga makubwa ya maisha. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel, kielelezo cha mshikamano wa kidugu.

Kanisa pia limeendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa maboresho ya huduma ya maji safi na salama kwa kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki  msingi za binadamu pamoja na kuwataka viongozi wa Serikali kuwa mstari wa mbele katika kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa linataka kuhakikisha kwamba, shule na taasisi za elimu zinakuwa ni mahali muafaka pa majiundo ya kiakili, kiutu, kimaadili na kitamaduni; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia sanjari na utume kwa vijana wa kizazi kipya. Kanisa linawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi na majiundo makini kwa njia ya Katekesi endelevu pamoja na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa.

Ibada kwa Bikira Maria kwa njia ya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Yagma, imekuwa ni fursa kwa waamini kufundwa chini ya shule ya Bikira Maria ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Hija hizi zimekuwa ni nafasi kwa waamini kukuza na kudumisha Sakramenti ya Upatanisho na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kuweza kujenga mahusiano yao na Kristo Yesu kwa njia ya sala na tafakari. Maaskofu wanaendelea kukazia umoja na mshikamano miongoni mwa Mapadre ili waweze kusaidiana, kutaabikiana na kutakatifuzana katika maisha na utume wao, kwa kujenga udugu unaopata chimbuko lake katika Ubatizo na Sakramenti ya Daraja Takatifu.

Kwa njia hii, mapadre wataweza kukabiliana barabara na changamoto katika maisha na utume wao! Malezi na majiundo makini ya Majandokasisi ni kati ya vipaumbele vya Maaskofu kwa ajili ya Seminari nchini humo. Waseminari wapewe nyenzo ya kutafakari, kuamua na kuitikia wito wa maisha na utume wa Kipadre kwa moyo wa shukrani na sadaka. Ili kufikia malengo haya, Maaskofu wameendelea kupeleka walezi bora na makini; ili kukuza urika kati ya Mapadre; Umoja na udugu wa Kisakramenti unaofumbatwa katika: ukarimu, upendo, kuheshimiana na kukosoana kidugu katika upendo na amani.

Maaskofu wanakazia utume wa Biblia pamoja na kuwataka waamini kujihusisha na vyama na mashirika ya kitume, kwa ajili ya maendeleo ya maisha yao ya kiroho, lakini hatima ya yote haya: ni umoja na mshikamano wa Kanisa la Kristo kama njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili ni changamoto inavyovaliwa njuga na Mama Kanisa. Kanisa pia limeendelea kuchangia katika huduma ya mama na mtoto pamoja na kuwajengea uwezo wanawake wa Burkina Faso kwa njia ya elimu makini.

Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo huko Burkina Faso na Niger, ili wote kwa pamoja waweze kushikamana ili hatimaye, kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo. Ujasiri unaofumbatwa katika ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi ni mambo msingi yanayopewa umuhimu wa pekee na Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger kwa wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.