2018-05-28 08:08:00

Papa Francisko: Vijana dumisheni uwepo wa Kristo; Umoja na Utume!


Vijana katika maisha na utume wao, wanapaswa kuzingatia mambo makuu matatu, kwanza kabisa ni: Uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha na historia ya kila kijana; pili, ni umoja na mshikamano utakaowawezesha vijana kuandika historia ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake; na tatu, ni utume  kwa kutambua kwamba, wameitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Hiki ni kiini cha ujumbe wa video kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliowatumia vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 kutoka Argentina, waliokuwa wanakutana mjini Rosario kuanzia tarehe 25-27 Mei 2018 kama sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa vijana nchini Argentina. Maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Pamoja nanyi, tupyaishe historia.”

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kuungana na familia ya Mungu nchini Argentina kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewawezesha kuamua na kutekeleza hija ya maisha ya kiroho, kwa furaha, imani na matumaini, ili kuweza kushirikishana yale yanayofumbatwa katika sakafu ya mioyo yao! Vijana wanapokutana, hapo wanaweza kuwasha cheche za imani na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Lakini, vijana wanapaswa kuwasha moto huu na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao na wala usiwe ni “moto wa mabua” bali moto wa “kifuu cha nazi”, unaowaka pole pole, lakini unadumu kwa muda mrefu!

Kwanza kabisa, Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, wanapaswa kutambua uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja nao, hata kama kuna wakati fulani katika maisha yao wanashindwa kutambua uwepo huo kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wawili wa Emau, walioshindwa kumtambua hata pale alipokuwa anawafafanulia Maandiko Matakatifu, lakini, mwishoni wakamtambua alipokua anamega mkate. Kristo Yesu, amejifanya rafiki, ndugu na mwandani wa maisha, kiasi cha kuwawezesha vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo unaomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha, katika mazingira na uhalisia wa maisha ya kila siku.

Ili kudumisha utamaduni wa upendo, kuna haja kwa vijana kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Kristo Yesu kwa njia ya: sala, tafakari ya Neno la Mungu na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Vijana wajenge moyo na utayari wa kuthubutu kukaa kimya mbele ya Sakramenti kuu, ili kumsikiliza Yesu anayezungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu! Si rahisi sana kwa vijana, ambao wana mambo mengi vichwani mwao, lakini, wakitaka kujua siri ya urembo, wajaribu na kweli wataona mafanikio katika maisha! Vijana katika safari ya maisha, wakati mwingine, wanakumbana na magumu na changamoto zinazowakatisha tamaa na kuacha madonda makubwa katika maisha yao.

Kristo Yesu ni Msamaria ambaye yuko tayari kuwaganga na kuwatibu; ili kuweza kupyaisha tena maisha yao, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, aliyekubali kupokea na kumwilisha mpango wa kazi ya ukombozi katika historia na maisha yake. Kristo Yesu, Msamaria mwema, anapenda kuwaendea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwafunulia Uso wa huruma na mapendo; kuwaganga na kuwaponya; yuko tayari kuinama na kuwanyanyua wale walioanguka na kupondeka moyo! Hii ndiyo changamoto hata katika maisha ya vijana, kuonesha moyo wa umoja na mshikamano ili kuwasaidia vijana wengine, wanaoogelea katika bahari ya shida na magumu na changamoto za maisha! Vijana wajenge utamaduni wa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu walau hata kwa dakika chache kila siku! Hapo watagundua “siri ya urembo”.

Pili, Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, wanaweza kujenga historia ya maisha na utume wao kwa kushirikiana na kushikamana na Kristo Yesu, kwani wao, ni sehemu ya muhimu sana ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa! Wao ni sehemu ya Jumuiya ya waamini, watu wa Mungu. Kumbe, vijana wanahamasishwa kushirikiana na kushikamana na wote kwa kutambua kwamba, Kanisa pia ni Jumuiya ya watakatifu waliotubu na kumwongokea Mungu; lakini pia ni Jumuiya ya watenda dhambi, wanaopambana na udhaifu wao ili kwa msaada wa neema ya Mungu, hata wao siku moja waweze kuwa ni watakatifu. Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango na uwepo wa vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wake, ndiyo maana ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili pamoja na vijana.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Duniani ambayo kwa Mwaka 2018, imeadhimishwa kwa ngazi ya kijimbo, na kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu”, vijana 350 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wameshiriki maadhimisho ya “Utangulizi wa Sinodi”, kwa kuwahusisha vijana kutoka katika dini na tamaduni mbali mbali. Zaidi ya vijana 15, 000 walishiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii. Baada ya kusali, kutafakari na kujadiliana, vijana wakatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Kumbe, huu ndio wakati uliokubalika kwa vijana wa Argentina kutoa pia mchango wao, utakaowasilishwa na Maaskofu mahalia wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Vijana. Baba Mtakatifu anawataka vijana kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya vijana kwa kushirikisha yale yanayowasibu kutoka katika undani wa maisha yao. Mama Kanisa anataka kujenga sanaa na utamaduni wa kujadiliana na kuwasikiliza vijana kutoka katika undani wa maisha yao, ili aweze kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha na utume wa vijana, ili kupyaisha imani na kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kama ilivyo kwa mambo ya Kompyuta na simu za viganjani, hata vijana wanapaswa kujipyaisha ili kuungana na Kristo Yesu, tayari kutembea katika mwanga wa Injili; kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, hii ndio dhamana wanayopaswa kuitekeleza na kwamba, anawaombea kwa moyo wake wote!

Tatu, baada ya kudadavua kuhusu uwepo endelevu wa Kristo na umoja, Baba Mtakatifu anasema vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utume wa Kanisa ambalo ni la kimisionari linalotumwa kutoka ili kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Hili ni Kanisa ambalo linajikita katika: dhana ya Msamaria mwema, Chemchemi ya huruma na mapendo; majadiliano katika ukweli na uwazi; sanaa na utamaduni wa kusikilizana. Kristo Yesu, anawaita na kuwatuma sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwabatiza na kuwazamisha watu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, katika utume, anawaaminia sana vijana, kwani wao ni jeuri ya Kanisa, jambo la msingi ni kuthubutu kutoka na kujiunga katika timu ya Yesu ili kuendeleza mashambulizi hadi kieleweke katika kuganga na kuponya madonda ya watu wengi duniani! Baba Mtakatifu anawaonya vijana kutokubweteka, kukaa na kuchungulia tu kutoka madirishani, bali waoneshe ari na moyo wa kuthubutu! Wakiwa wameungana na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake wapandikize mbegu ya matumaini ili kupyaisha historia na maisha ya binadamu! Vijana ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Ni kesho yenye msingi wa matumaini na wala si katika ndoto za mchana! Ni kesho inayojengwa katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, jamii na historia ya watu husika. Vijana wanayo dhamana ya ujenzi wa jamii yao.

Mwishoni mwa ujumbe wake kwa njia ya video kwa vijana wa Argentina, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maia wa Rozari Takatifu, ili aweze kuwafunda katika shule ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. Bikira Maria, daima yuko tayari kuwasaidia wale wote wanaokimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama; ni  Mama na mfano bora wa maisha ya imani, mwaliko kwa vijana kumwendea ili aweze kuwafunda vyema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.