2018-05-26 15:44:00

Wakristo na Wabudha pambaneni kwa dhati kabisa na rushwa na ufisadi


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Vesakh/Hanamatsuri kwa ajili ya waamini wa dini ya Kibudha, inayoadhimishwa na nchi nyingi tarehe 29 Mei 2018, linawaalika Wakristo na Mabudha kushikamana kwa dhati kabisa katika mapambano dhidi ya utamaduni wa rushwa na ufisadi. Siku kuu hii iwe ni chemchemi ya furaha na amani kwa watu wote wenye mapenzi mema, sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema, kwa mwaka 2018 linapenda kutafakari pamoja na waamini wa dini ya kibudha mchakato wa mapambano dhidi ya utamaduni wa rushwa na ufisadi unaojikita katika matumizi mabaya ya madaraka kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi. Hali hii inajionesha katika shughuli za serikali na hata katika sekta binafsi, kiasi cha kugeuka kuwa ni kashfa ya kimataifa katika ulimwengu mamboleo. Kutokana na changamoto hii, Umoja wa Mataifa umetenga tarehe 9 Desemba kuwa ni Siku ya Kupambana na Rushwa Duniani. Kutokana na kuenea kwa rushwa na ufisadi, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya mawasiliano ya jamii, wananchi na wapenda maendeleo sehemu mbali mbali za dunia wanapaswa kuunga mkono juhudi hizi ili kutokomeza rushwa na ufisadi “unaopekenyua” maisha ya watu wengi duniani. Kwa upande wao, viongozi wa kidini wanapaswa kujizatiti kujenga na kudumisha utamaduni wa ukweli na uwazi ili kudumisha utawala bora unaosimikwa katika misingi, kanuni na sheria.

Nia ya Sala ya Jumla ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Februari, 2018 ilikuwa inaongozwa na kauli mbiu “Tuseme hapana kwa rushwa na ufisadi”. Rushwa ni saratani inayoenea kwa haraka sana kati ya wanasiasa, wafanyabiashara na hata kati ya viongozi wa Kanisa. Lakini, ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Baba Mtakatifu anasema, dhana ya uongozi inapaswa kuchukuliwa kuwa ni sehemu muhimu sana ya huduma kwa watu wa Mungu.

Rushwa na ufisadi vinapata chimbuko lake anasema Baba Mtakatifu Francisko katika kiburi na majivuno ya binadamu, wakati ambapo huduma makini, inamnyenyekesha kiongozi, kiasi kwamba, anajisikia kuwa ni chombo na shuhuda wa huduma ya upendo kwa jirani zake! Ujumbe huu ambao umetiwa sahihi na Kardinali Jean Louis Tauran, ambaye ni Rais pamoja  na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza, unaendelea kudadavua kwa kukazia kwamba, rushwa na ufisadi vinapaswa kuhesabiwa kuwa ni ugonjwa unaosababisha madhara makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni ugonjwa unaochafua jamii kwa kupandikiza sumu kali ya: uchu na tamaa; chuki, hali ya kukata tamaa ambayo inawatumbukiza watu katika ujinga. Waamini wa dini hizi mbili wanapaswa kujizatiti ili kung’oa kabisa sumu hii, kwa kuzingatia sheria kanuni maadili na utu wema; kwa kuheshimu mali ya watu wengine na kurudisha mali ambayo pengine watu wamejitwalia kinyume cha sheria kama anavyofundisha Budha. Mafundisho ya dini ya Kibudha yanakataza kabisa tabia ya rushwa na ufisadi na kuwakemea watu ambao wanaogelea katika tabia. Lakini, ikumbukwe kwamba, dini zote duniani zinakemea sana tabia ya rushwa na ufisadi!

Kwa masikitiko makubwa, Baraza la Kipapa linakiri kwamba, hata waamini wa dini hizi mbili wamejikuta wakitopea katika tabia ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, hali inayopelekea utawala mbovu; hatari ya maisha kwa watu wengi, uchumi kudumaa, ukosefu wa elimu na huduma bora ya afya; uharibifu wa miundo mbinu na mazingira; sanjari na kuhatarisha amani na usalama wa jamii. Ni kashfa kubwa kwa wananchi kuwaona viongozi waliobobea katika rushwa na ufisadi wakitanua, huku wakishindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao pamoja na kuwawajibisha watu wanaotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi wa mali ya umma! Wakati mwingine, rushwa inachochewa na watu wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani wanaotaka kuharibu mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema, rushwa na ufisadi kamwe, hauwezi kutokomezwa kwa watu kukaa kimya, bali kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati unaofanyiwa kazi, ili kuhakikisha kwamba, unatekelezwa kwa dhati, ili hatimaye, rushwa na ufisadi, viweze kupewa kisogo! Wakristo na Wabudha wanapaswa kujizatiti kikamilifu katika mafundisho ya dini zao kwa kuzingatia kanuni sheria maadili; kwa kuwahamasisha waamini kuwa wakweli na waaminifu; kwa kukazia misingi ya ukweli na uwazi; usawa na uwajibikaji.

Lengo la pamoja ni waamini wa dini hizi mbili kushikamana na kuendelea kushirikiana na vyombo vya upashanaji habari pamoja na jamii katika ujumla wake ili kuzuia na kupambana na rushwa katika mifumo mbali mbali. Ni wajibu wa waamini wa dini hizi mbili kuendelea kuragibisha uelewa wa madhara ya rushwa na ufisadi katika jamii, ili kuwasaidia wafanyakazi na watumishi wa umma kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu bila kuelemewa na ukabila, udini, mahali anapotoka mtu, chama au itikadi yake. Wananchi wote wafunzwe na kufundwa, lakini zaidi wanasiasa na wafanyakazi wa umma kuhakikisha kwamba wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa weledi, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji kama sehemu muhimu sana ya kupambana na rushwa pamoja na ufisadi!

Mali ya rushwa itaifishwe na kurejeshwa kwa umma na wahusika wafikishwe kwenye mkondo wa sheria. Wanawake wahamasishwe zaidi na zaidi kushiriki katika masuala ya kisiasa; watu wenye tuhuma za rushwa na ufisadi wasipewe dhamana ya uongozi! Wananchi waelimishwe umuhimu wa ukweli na uwazi, utawala wa sheria na uongozi bora na makini ili waweze kuwajibika kwa ajili ya maendeleo ya wengi! Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Vesakh/Hanamatsuri kwa ajili ya waamini wa dini ya Kibudha, kwa kuwataka waamini wote kujizatiti katika familia, taasisi za kijamii, katika masuala ya kisiasa, kiraia na kidini kujenga mazingira ambayo kamwe hayatakuwa na harufu ya rushwa na ufisadi, ili kukuza na kudumisha fadhila ya unyofu na uaminifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.