2018-05-26 14:23:00

Udhibiti wa silaha za maangamizi,kawaida na kiteknolojia bado ni changamoto!


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza mwelekeo wake mpya  kuhusu udhibiti wa silaha katika juhudi za kutokomeza  silaha za nyuklia  pamoja na silaha zingine zinazoweza kusababisha maangamizi dunia  kutokana na makosa, iwe  ya kiufundi, kielektroniki au ya kibinadamu.  Bwana Antonio Guterres akizindua ajenda yake yenye kauli mbiu “kutunza usalama katika wakati  wetu pamoja”, kwenye  Chuo Kikuu cha Geneva, huko Uswiss, amesema, Umoja wa Mataifa uliundwa  kwa lengo la kuondoa vita inayotumika kama chombo cha sera ya kigeni.  Lakini kwa  miongo saba sasa imepita, dunia yetu bado inaedndelea na hatari zaidi ya ilivyokuwa kabla, na kwa njia hiyo amefafanua kwamba, udhibiti wa silaha unazuia  na kukomesha vita, udhibiti ndio jibu kwa misingi yetu,ambapo anasema, uzinduzi huo wa ajenda umekuja kwa wakati udhibiti wa silaha umekuwa kama wimbo wa kila siku, kwa maana wakati mwingine kuhusu Iran na Syria,na siku nyingine kuhusu rasi ya Korea; lakini pamoja na hayo anaunga mkono juhudi za maendeleo endelevu kwa matarajio ya mshimano na ushirikiano katika kuunga mkono nchi zote duniani. 

Aidha pamoja na hayo, Ajenda hiyo inalenga vipaumbele vitatu, kwanza silaha za maangamizi, silaha za kawaida na teknolojia mpya kuhusu vita. Bwana Guterres amesisitiza katika hotuba yake kuwa, udhibiti wa silaha za nyuklia,na silaha za kemikali na  za kibayolojia unaweza kuokoa binadamu, akibainisha kwamba, bado silaha takriban 15,000 za nyuklia zimehifadhiwa sehemu mbalimbali duniani na ziko tayari kutumiwa wakati wowote ule. Kadhalika amesema, mataifa yaliyo na  silaha za nyuklia yana wajibu wa kwanza kuepusha dunia na janga hili.

Kutokana na mantiki hiyo ameziomba nchi za Marekani na Urusi kuondoa tofauti zao ili zitafute suluhisho la  mgogoro kuhusu  mkataba wa makombora ya masafa ya kati, yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia. Aidha ameziomba pia kurefusha mkataba mpya wa kuzidi kupunguza silaha nzito ambao pia unahusu silaha za kinga  kwa kifupi START, ambao unakaribia kumalizika katika kipindi cha miaka mitatu kutoka sasa. Katibu Mkuu pia amezitaka zichukue hatua mpya za kupunguza mrundikano wa silaha za nyuklia na kwamba, mbali na watu wengi kuuawa na kujeruhiwa, migogoro inasababisha watu wengi kuacha nyumba zao, wakati mwingine kukosa chakula, huduma za kiafya, elimu pamoja na mbinu za kuendeleza maisha yao.

Ametoa mifano kadhaa kwamba hadi mwisho wa mwaka 2016 zaidi ya watu milioni 65 wamehama makazi yao kutokana na migogoro ya kivita, ghasia na mateso. Kwa njia hiyo amethibitisha kuwa, juhudi zake zitakuwa zinaegemea zaidi katika ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu, ambayo ndio msingi wa dunia yenye amani, maendeleo na afya bora. Amemalizia akikazia kuwa,  udhibiti wa silaha utaokoa maisha na zaidi ya yote utaokoa raia wa kawaida ambao wanaendelea  kuteseka kutokana na migogoro ya kivita bila hatia.

Na Sr Angela Rwezaula 
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.