2018-05-26 08:29:00

Sherehe ya Utatu Mtakatifu: Umoja, Ukuu, Uweza na Utakatifu wa Mungu


Utangulizi: Mungu Mmoja, wa kweli na wa pekee amejifunua katika Nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ndilo fumbo la Utatu Mtakatifu ambalo Mama Kanisa analiadhimisha katika dominika ya leo. Hili ni fumbo la msingi la imani na la maisha ya kikristo, ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe na ni chanzo cha mafumbo mengine yote ya imani.

Masomo kwa ufupi: Somo la Kwanza (Kumb. 4:32-34, 39-40) limechukuliwa kutoka hotuba ya Musa kwa waisraeli. Ni hotuba anayoitoa Nabii, Mwalimu na kiongozi wa jamii kufundisha, kukumbusha, kuhimiza na kutoa mwelekeo kwa wana wa israeli. Katika hotuba hiyo, Musa anasisitiza juu ya ukuu na upekee wa Mungu. Anawaonesha waisraeli namna gani Mungu wao alivyo mkuu na alivyo wa pekee; “ndiye Mungu katika mbingu juu na katika nchi chini, hapana mwingine”. Anawakumbusha pia namna ambavyo Mungu huyu amewafanyia hisani ya pekee. Amewachagu kuwa watu wake na kuwa urithi wake, kitu ambacho hakuwahi kukifanya kwa taifa lolote lile na tena wao wameisikia sauti yake, kinyume na wote walioisikia wakafa, wao wanaishi. Kisha anawaasa wazishike amri zake ili wazidi kupata neema zake waingiapo katika nchi ya ahadi, Kanaani.

Somo la pili (Rum. 8: 14-17) Mtume Paulo anazungumzia juu ya nafasi ya Roho ya Mtakatifu kwa wote wanaoamini. Anasema, Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya kuwaongoza. Anawaongoza kama vile mkufunzi awaongozavyo wale wanaofanya mafunzo hatua kwa hatua. Anawaongoza kama msafiri anavyoongozwa na yule aijuaye njia. Anaongeza Mtume Paulo kuwa Roho anawaongoza watu si kama aongozaye mateka bali kama aongozaye wana ambao ni warithi pamoja na Kristo. Wana walio na hadhi, na nafasi ya pekee kwa Mungu kwa sababu ya imani yao.

Injili (Mt. 28: 16-20) Yesu anawatokea wanafunzi wake baada ya ufufuko. Katika muktadha wa dominika ya leo, msisitizo wa somo hili upo katika utume ambao Yesu anawapa wanafunzi wake. Utume wa kwenda ulimwenguni kote na kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wake. Utume huo anaowapa mwenyewe ameupokea kutoka kwa Baba. Anasema “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”. Na kama yeye alivyotumwa vivyo hivyo na yeye anatuma. Ndiyo maana kwa jina na mamlaka ya Yesu mitume nao wanapata nguvu na mamlaka yale yale kutoka kwa Baba kwa njia ya Yesu Kristo wanapotekeleza utume wao hadi ukamilifu wa dahari.

Somo la kwanza limeonesha nafasi ya Mungu Baba, umoja na ukuu wake toka mbinguni juu hadi duniani chini; Somo la Pili likaonehsa nafasi ya Roho Mtakatifu; injili inaonesha nafasi ya Mwana- Bwana wetu Yesu Kristo. Ni katika injili pia tunaona nafsi zote tatu zinatajwa pamoja katika ubatizo Yesu anaowaagiza wanafunzi wake kuufanya “mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, sherehe tunayoadhimisha leo ni sherehe inayogusa fundisho kuu juu ya Mungu mwenyewe. Ni fundisho la imani na hapohapo ni fumbo, kwamba Mungu wa kweli na wa pekee ni mmoja katika nafsi tatu ambazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Karibu sote katika shule za Msingi tumejifunza mafumbo katika somo la kiswahili. Tukaona kuwa katika fumbo kunakuwa na tungo yenye kitu au mantiki iliyofichwa na inayohitaji jibu maalumu kutoka upande wa pili, upande wa anayetakiwa kulifumbua fumbo hilo. Ili kulifumbua fumbo ilikuwa inahitajika kufikiria sana kung’amua mantiki ya maneno. Sasa kama katika mafumbo yetu hali iko hivyo, itakuwaje katika mafumbo ya kimungu?, tena katika fumbo kama hili la Utatu Mtakatifu linaloguza umungu wenyewe? Ni hapa tunaona kuwa Kanisa linaleta kwetu fumbo la Utatu Mtakatifu kama alivyolifunua Mungu mwenyewe si ili tulifumbue bali tuamini juu ya Utatu Mtakatifu na ili tupokee fundisho lake kwa ajili ya wokovu wetu.

Tunaamini juu ya fumbo la Utatu Mtakatifu kwa sababu Mungu mwenyewe amelifunua kwa namna ya pekee katika Maandiko Matakatifu kuanzia Agano la Kale hadi Agano Jipya. Katika Agano la Kale ufunuo wa Utatu Mtakatifu unapatikana si kwa namna ya moja kwa moja bali katika viashiria ambavyo tangu mwanzo Mababa wa Kanisa wamevihusisha na ufunuo wa Utatu Mtakatifu. Kwanza ni pale ambapo Mungu anaongea kwa nafsi ya wingi katika utendaji wake wa kimungu. Mfano katika uumbaji anasema “na tumfanye mtu kwa mfano wetu” (rej. Mwa. 3:22, 11:7). Pili katika vifungu vinavyotabiri juu ya Masiha (unabii wa kimasiha) tofauti za nafsi zinadokezwa. Katika Zaburi  2 “Bwana amemwambia Bwana wangu ndiwe mwanangu mimi leo nimekuzaaa” Na katika Is. 7: 14 utabiri kuhusu Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi. Agano la Kale pia linazungumza juu ya Roho wa Mungu kama nguvu inayotoka kwa Mungu (Mwa. 1:2, Zab 32:6).

Agano Jipya linadhihirisha zaidi nafsi tatu za Mungu. Katika kupashwa habari Birikira Maria kuwa Mama wa Mungu malaika anamwambia “Roho Mtakatifu atakujilia na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kwa kivuli chake na hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu Mwana wa Mungu” (Lk. 1:34). Hapa anatajwa Roho Mtakatifu, anatajwa Aliye Juu na anatajwa Mwana wa Mungu. Katika karamu ya mwisho, Kristo mwenyewe anaahidi kumtuma Roho Mtakatifu, Roho ambaye anawashukia mitume siku ya Pentekoste (Yoh. 14:16; Mdo. 2). Na hatimaye kanuni ya ubatizo watakaoutoa Mitume kama alivyowaagiza Yesu ni kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Nafsi tatu za Mungu mmoja.

Fumbo hili pia linaweka mbele yetu fundisho kuu juu ya ukuu wa Mungu tunayemwamini, Mungu anayeyazunguka maisha yetu tangu mwanzo, kuyaongoza na kuyaelekeza kuufikia mwisho aliokusudia mwenyewe. Mungu Baba aliye muumba ndiye mwanzo na asili ya vyote. Mwanzo wa maisha yangu na ya ulimwengu mzima; kila wakati anaendelea kuyaumba upya maisha yafanane na sura na mfano wake. Mungu Mwana ndiye Mkombozi, ndiye anayetuokoa kutoka upotevu wetu na kuturudisha katika nuru na hadhi ya kuumbwa kwetu. Mungu Roho Mtakatifu ndiye mfariji, anayetutakasa, kutuongoza na kutupa nguvu. Mbele ya ufunuo huu wa Utatu Mtakatifu, mbele ya ukuu wa Mungu upitao ufahamu wetu tunapata nafasi leo ya kujihoji juu ya imani yetu kwa Mungu. Ni Fumbo linalotualika kuiimarisha imani yetu. Na kama alivyosali mbele ya Yesu baba mwenye mwana mgonjwa nasi leo tunasali “Naamini Bwana, nisaidie kutokuamini kwangu” (Rej. Mk. 9:24).

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS.
All the contents on this site are copyrighted ©.