2018-05-26 14:55:00

Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Mafao ya wengi ni ajenda ya kiekumene


Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako tarehe 13 Juni 1993, kumbe, mwaka 2018, unaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Lengo la mfuko huu ni kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbali mbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol amekuwepo na ameshiriki katika kuchangia mada kwa kukazia “Mafao ya wengi kama ajenda ya pamoja kwa Wakristo wote”. Kwa namna ya pekee kabisa amejikita katika sekta ya uchumi na ekolojia; Sayansi na teknolojia; jamii na siasa. Mshikamano na mafungamano ya kiekumene ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko; chemchemi ya furaha ya Injili na wokovu kwa walimwengu. Tunu msingi za Kiinjili hazina budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kijamii kwa kuongozwa na mambo yafuatayo: utu na heshima ya binadamu; mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kama kanuni zinazoweza kutumiwa na Kanisa ili kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Familia ya Mungu haina budi kujenga utandawazi na utamaduni wa mshikamano.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza akidadavua kuhusu sekta ya uchumi na ekolojia, anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la umaskini wa hali na kipato; baa la njaa na upungufu mkubwa wa chakula pamoja na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Matokeo yake utu na heshima ya binadamu vimewekwa rehani na badala yake, watu wanatafuta faida kubwa hata kwa gharama ya maisha ya watu na utamaduni wa mshikamano. Mafanikio makubwa yaliyokuwa yamepatikana katika masuala ya kijamii, yanaendelea kuporomoka kila kukicha na kwamba, pengo kati ya maskini na matajiri limeongezeka maradufu. Urithi, amana na utajiri wa maisha ya kiroho, umenyofolewa na kutupwa “mahali kusikojulikana.”

Changamoto za kiekolojia ni matokeo ya sera na mikakati ya uchumi usiojali; uchumi unaongozwa kama “roboti”, ili kupata faida kubwa, lakini madhara yake ni makubwa katika mchakato mzima wa uharibifu wa mazingira nyumba ya wote! Waathirika wakuu ni “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”. Mambo yote haya yanachangia kubomoa mshikamano na mafungamano ya kijamii, hatari kwa siku za usoni!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, badala ya kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, yamejenga moyo wa uchoyo na ubinafsi na madhara yake ni makubwa katika maisha ya watu: yaani maana ya maisha na mahitaji msingi ya binadamu yamebadilika sana. Teknolojia kwa sasa imegeuka kuwa kama mungu mdogo! Computer leo hii ni chanzo cha: habari, mawasiliano, maendeleo na fursa za ajira.

Matokeo yake ni kuvunjika kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; vita, uvunjifu wa haki msingi za binadamu, upweke hasi pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani! Vyombo vya mawasiliano ya jamii vimekuwa mstari wa mbele kuwapotosha watu; kwa kujikita katika ubinafsi na uchoyo; pamoja na ukosefu wa haki jamii. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamepelekea kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu! Mahusiano na mafungamano ya watu ndani ya jamii, yamekuwa baridi sana, kiasi hata Mwenyezi Mungu kukosa nafasi katika maisha ya watu; ustawi na maendeleo ya wengi; hatari kwa mshikamano wa kijamii.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, hata katika sekta ya jamii na siasa, ubinafsi na uchoyo vinatawala, kiasi cha baadhi ya watu kudhani kwamba, wanajitosheleza wenyewe na wala hawahitaji msaada kutoka kwa wengine. Hawa ni watu ambao wametumbukia katika uchoyo, kumbe, upendo, mshikamano na hali ya kushirikisha, havina tena nafasi. Haki msingi za binadamu zinaendelea kupewa tafsiri potovu kwa kukazia haki binafsi; dhidi hata ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililotolewa na Umoja wa Mataifa.

Kumbe, Wakristo wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu na heshima ya binadamu; kwa kutangaza na kushuhudia amana na utajiri wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; kwa kuonesha umuhimu na nafasi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Umefika wakati wa kumwilisha imani katika matendo; utu na heshima ya binadamu. Kwa kusimama na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Kanisa lishinde kishawishi cha uchu wa mali na madaraka; kwa kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na huduma; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kukuza na kudumisha uhuru; majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi kama chachu ya maendeleo endelevu. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anahitimisha mchango wake kwa kusema kwamba,  maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yawawezeshe waamini kuyatakatifuza mazingira; kwa kujenga umoja, mshikamano na uhuru wa kweli ili kupambana na umaskini wa hali na kipato; sanjari na kuboresha hali ya maisha ya watu na kujenga utamaduni wa huduma na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.