2018-05-25 15:02:00

Papa Francisko: Waamini shuhudieni: Ukuu, Uzuri na Utakatifu wa Ndoa


Familia ni kitovu cha elimu ya uraia mwema. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 25 Mei 2018 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Ibada hii imehudhuriwa na wanandoa saba waliokuwa wanamshukuru Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 na wengine 25 tangu walipofunga Ndoa, matendo makuu ya Mungu katika maisha! Baba Mtakatifu alikuwa anafafanua kuhusu Ndoa na Talaka kama Mafarisayo walivyotaka kumtega kwa kumuuliza swali tete kuhusu imani, wakidhani kwamba, Yesu alikuwa ameandaa majibu mepesi mepesi ya “Ndiyo” au “Hapana” katika imani. Ikumbukwe kwamba, maisha ya Kikristo ni mwaliko kwa waamini kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kama kielelezo na ushuhuda wa: Ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia.

Yesu katika ufafanuzi wake, anawarejesha Mafarisayo katika chimbuko la ndoa, kadiri ya mpango wa Mungu, aliyewaumba mwanaume na mwanamke kwa mfano na sura yake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; nao wawili watakuwa mwili mmoja. Basi kile alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Yesu anaweka kando matatizo na changamoto za ndoa na familia na kujikita katika uzuri na utakatifu wa Ndoa, kama chemchemi ya neema na sehemu ya mchakato wa maisha ambamo mwanandoa wanasaidiana na kutakatifuzana!

Baba Mtakatifu amewauliza wanandoa waliokuwepo hapo kama kweli walikuwa bado wanapendana hata baada ya kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 na wengine 25, wote wakaangaliana na kujikuta wakibubujikwa na machozi ya furaha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maisha ya ndoa, kuna matatizo, raha na karaha zake! Huko ni patashika nguo kuchanika, lakini yote haya ni mambo mpito, jambo la msingi ni kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwani Ndoa ni Sakramenti ya Kanisa kwa ajili pamoja na Kanisa na kwamba, upendo wa dhati kabisa unawezekana hata katika ulimwengu mamboleo.

Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanadumu katika nia njema, upendo wa dhati na uaminifu endelevu katika taabu na raha; katika magonjwa na afya; wapendane na kuheshimiana siku zote za maisha yao! Huu ndio uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni ushuhuda wa Injili ya familia unaotangazwa katika ukimya. Jubilei ya Miaka 50 au 25 ya Ndoa si habari wala mali kitu kwa baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, wao wanasubiri kashfa! Wametalakiana na kutengana, eti hii ndiyo “habari ya mujini” anasema Baba Mtakatifu Francisko. Inawezekana wanandoa kutengana ili kuepuka maafa na majanga makubwa katika familia! Ikumbukwe kwamba, uvumilivu ni fadhila muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake akiliombea Kanisa na jamii katika ujumla wake kutambua na kuheshimu uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; mfano na sura ya Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.