2018-05-25 12:33:00

Maadhimisho ya Siku ya Afrika yanazingatia dira ya maendeleo 2063!


Siku ya Afrika inakumbusha kuundwa kwa Umoja wa Afrika tangu 25 Mei 1963, kwa maana hiyo ni  miaka 55  iliyopita ya kuzaliwa Umoja wa nchi huru za Afrika, ambao sasa ni Muungano wa Afrika, (AU). Katika kilele hicho hata Bwana Guterres amesema kwamba, kwa sasa Afrika inazidi kuongeza kasi ya kujiendeleza kwa kuzingatia dira yake ya maendeleo kufikia 2063. Akizungumzia suala hili hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres amesema kuwa, kama ambavyo jina limebadilika, ndivyo  hivyo, hali ya bara la Afrika inazidi kubadilika. Kwa kusisitiza ameongeza, hivi sasa kuna mafanikio makubwa kwa kutaja uzinduzi wa hivi karibuni wa eneo la soko huru barani humo ambapo litatochea ukuaji wa kiuchumi kwa wakazi bilioni 1.2 wa bara hilo na hatimaye kutokomeza umaskini. Kama hiyo haitoshi pia amegusia kasi ya ukuaji wa ujasiriamali, idadi ya watoto wanaopata elimu pamoja na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga huku wanawake wengi zaidi wakichaguliwa kuwakilisha jamii zao kwenye mabunge.

Hakukosa kugusia pia suala la amani na maendeleo endelevu akifananisha kama Zinduna na Ambari kwa maana vinakwenda pamoja, hakuna kinachoweza kufanikiwa bila kujumuisha mwenzake! Bwana Guterres amesema Umoja wa Mataifa utashirikiana na ule wa Afrika (AU) kusaidia mpango wake wa kuhakikisha mapigano barani humo yanasitishwa ifikapo mwaka 2020 huku akipaza sauti zaidi kwamba, katika siku hii ya Afrika, anasihi mataifa yote yaunge mkono azma ya Afrika yenye amani na ustawi. Kilicho bora kwa Afrika ni bora kwa dunia nzima. UN imedhamiria kuunga mkono juhudi za Afrika. Kwa mantiki hiyo taasisi hizi mbili mwaka jana zimetia saini makubaliano kuhusu mfumo wa amani na usalama pamoja na utekelezaji wa ajenda 2063 ya AU na ile ya UN ya 2030.

Aidha katika kuadhimisha siku ya Afrika, lugha za asili za Afrika nazo zimepigiwa debe ili kutambuliwa zaidi miongoni mwao ni lugha ya Kiswahili ambayo barani Afrika imekuwa pekee inaongoza kwa kuzungumzwa na watu wengi zaidi, idadi ikitajwa kuwa ni zaidi ya watu milioni 200. Akizungumzia nafasi ya lugha ya kiswahili katika kuchagiza maendeleo barani humo, Profesa Aldin Mutembei wa Taasisi ya Taaluma za lugha ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, (TATAKI) Tanzania, amesema hilo linawezekana iwapo vijana watapatiwa fursa ya kusoma masomo ya sayansi na teknolojia kwa lugha yao ya asili ambayo ni Kiswahili.

Lakini pamoja na hayo Profesa Mutembei ameonesha jambo fulani ya kwamba, ingawa baadhi ya waswahili wanapuuza lugha hiyo, mataifa mengine Afrika kwa kutambua umuhimu wake, wanaienzi sana  na punde lugha hiyo itakuwa na wabobezi wengi zaidi. Hivi karibuni ilielezwa kuwa, lugha ya Kiswahili inaongoza kwa kuwa lugha ya asili inayozungumzwa na watu wengi barani Afrika ikifuatiwa na kihausa halafu kiyoruba.


Na Sr Angela Rwezaula
Vatican News

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.