2018-05-25 06:59:00

Benki ya Vatican yaendelea kujiimarisha zaidi katika huduma makini!


Usimamizi wa fedha na mali ya Kanisa katika: ukweli, uwazi, uadilifu na weledi ni kati ya mambo msingi yanayoendelea kupewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko ili kweli rasilimali fedha iweze kutumika kimailifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati uchumi na maendeleo na kwamba, fedha ni chombo cha huduma ili kujibu kilio cha maskini na kuzima kiu ya maendeleo na wala haipaswi kuwa ni mtawala!

Benki ya Vatican, maarufu kama “Institute for Work of Religion” IOR, imechapisha taarifa ya fedha kwa mwaka 2017 baada ya kukaguliwa na hatimaye kuthibitishwa na Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte & Touche S.p.A. Benki imeendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia kanuni maadili na uadilifu mkubwa, kama chombo cha huduma ya kifedha cha Kanisa Katoliki chini ya usimamizi wa Vatican. Ni Benki inayotekeleza huduma yake katika nchi 112. Taarifa ya fedha imepitiwa na kuidhinishwa kwa kauli moja na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Vatican.

Takwimu zinaonesha kwamba, Benki hii inatoa huduma kwa wateja 15, 000 waliowekeza kiasi cha Euro bilioni 5.3. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Euro bilioni 3. 5 ni amana inayotunzwa na uongozi wa Benki. Benki imefanikiwa kupata kiasi cha Euro milioni 31.9. Itakumbukwa kwamba, taarifa ya mwaka 2016 ilionesha faida ya kiasi cha Euro milioni 36 pamoja na kiasi cha Euro milioni 13 zilizokuwa zimetolewa kwa dharura. Faida kubwa ya Benki ya Vatican inatokana na vitega uchumi vyake ambavyo ni kiasi cha Euro milioni 44.3.

Sera na mikakati ya uwekezaji wa Benki ya Vatican imeendelea kuwa makini kutekeleza mbinu mkakati uliopangwa miaka kadhaa iliyopita. Benki imendelea pia kubana matumizi kwa kiasi kikubwa kutoka kiasi cha milioni 19.1 katika kipindi cha mwaka 2016 hadi kiasi cha Euro milioni 18.7 kwa mwaka 2017. Shughuli za uwekezaji na utekelezaji wa miradi mbali mbali ya Benki ya Vatican unafuata na kuzingatia sheria kanuni na maadili ya Kanisa Katoliki. Mkazo umewekwa zaidi katika: maisha, utu na heshima ya binadamu kama vigezo muhimu katika kupanga na kuchagua miradi ya kuwekeza.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni kati ya mambo ambayo pia yanazingatiwa na Benki ya Vatican katika kuamua ni mahali gani pa kuwekeza, ili kuendeleza uwajibikaji wa kijamii kama sehemu ya urithi mkubwa wa Mafundisho Jamii. Haki msingi za binadamu, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma pamoja na huduma makini kwa maskini, ni mambo yanayozingatiwa sana. Katika kipindi cha Mwaka 2017, Benki pia imesaidia kugharimia miradi mbali mbali ya kijamii, kwani fedha inapaswa kuwa ni chombo cha huduma kwa maskini na wala si vinginevyo!

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.