2018-05-24 15:47:00

Jumuiya ya Papa Yohane XXIII inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50


Jumuiya ya Papa Yohane XXIII inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa na Don Oreste Benzi kunako mwaka 1968. Tangu wakati huo anasema Bwana Giovanni Paolo Ramonda, Jumuiya yake ambayo imeenea katika nchi 42, Tanzania ikiwemo, imekuwa ni kama hospitali katika uwanja wa mapambano sehemu mbali mbali za dunia. Kwa muda wa siku tatu, kuanzia Ijumaa tarehe 25 hadi Jumapili tarehe 27 Mei, 2018 wanachama wa Jumuiya ya Papa Yohane XXIII wanafanya mkutano mkuu unaopambwa kwa uwepo na ushuhuda makini wa Kardinali  Ernest Simoni anayetarajia kuadhimisha miaka 90 ya maisha, mwezi Oktoba, 2018.

Huyu ni Padre kutoka nchini Albania, aliyesababisha Baba Mtakatifu Francisko kububujika machozi ya furaha alipokutana naye mubashara huko Albania, kama alama ya shukrani kwa ushuhuda, udumifu na uaminifu wake kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kuweza kuhimili: mateso, nyanyaso na kifungo cha miaka 28 jela na kazi ngumu! Hata alipokuwa kifungoni, aliendelea kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa uficho. Akawa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wafungwa wengi waliotubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao.

Bwana Ramonda ambaye ni Rais wa Jumuiya ya Papa Yohane XXIII anasema, changamoto kubwa mbele yao kwa wakati huu, ni kulisaidia Kanisa kutoka kifua mbele ili kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu; changamoto ambayo imevaliwa njuga na Jumuiya hii katika maisha na utume wake kwa muda wa miaka 50, matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Maadhimisho haya yanahudhuriwa na Askofu Livio Corazza wa Jimbo Katoliki Forli na Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo la Cesena-Sarsina, Italia.

Kardinali Ernest Simon anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Mkesha wa Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Jumamosi, tarehe 26 Mei 2018. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Papa Yohane XXIII ni fursa makini kwa wanachama wake kuweza kukutana. Itakumbukwa kwamba, hii ni Jumuiya inayotekeleza dhamana na utume wake miongoni mwa walemavu, waathirika wa utumwa mamboleo, wafungwa waliomaliza adhabu zao na kwa sasa wanaendelea na malezi, ili kuandika kurasa mpya katika maisha yao. Ni Jumuiya inayojisadaka kwa ajili ya maskini, watu wasiokuwa na makazi maalum; wakimbizi na wahamiaji. Umoja, upendo na mshikamano wa kidugu ndiyo ngao ya maisha na utume wao. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Jumuiya imeweza kujenga nyumba zaidi ya 500 kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.