2018-05-23 14:53:00

Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo! Siku ya Kuombea China!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 23 Mei 2018, amewakumbusha waamini kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, anayeheshimiwa sana kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Sheshan, huko Shanghai, nchini China. Hii ni siku maalum ambayo, Wakristo wote wanaungana kiroho na waamini Wakatoliki wanaoishi nchini China ili kusali na kuwaombea. Kanisa linawaombea ili, waweze kuishi imani kwa ukarimu na utulivu wa ndani; kwa amani na upatanisho; huku wakiwa na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Wakristo nchini China kwamba, Kanisa zima linasali kwa ajili pamoja nao, ili hata katika “litania” nyingi za mateso na mahangaiko, waendelee kujitoa na kujiaminisha katika kutekeleza mapenzi ya Mungu! Bikira Msaada wa Wakristo daima, atawapatia msaada na tunza ya upendo wake wa kimama! Itakumbukwa kwamba, Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, ilianzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815. Huu ulikuwa ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Bikira Maria msaada wa Wakristo, ili awasaidie kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kunako mwaka 2001 Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mama na msimamizi wa Familia ya Mungu nchini China.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akatangaza tarehe 24 Mei ya kila Mwaka kuwa ni Siku ya Kuombea China. Tangu wakati huo, Kanisa zima linakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa ajili ya familia ya Mungu nchini China; siku ambayo China pia inaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Sheshan. Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo ilianzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815. Huu ulikuwa ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Bikira Maria msaada wa Wakristo, ili awasaidie kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kunako mwaka 2001 Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mama na msimamizi wa Familia ya Mungu nchini China.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.