2018-05-23 16:57:00

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu!


Mpendwa Msikilizaji wa Vatican News! Utangulizi wa Sala ya Ekaristi Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu hutuambia maneno yafuatayo: “Wewe pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika utatu wa Mungu mmoja. Mambo tunayoyasadiki juu ya utukufu wako, kwa sababu ya ufunuo wako, twayasadiki pia juu ya Mwanao na juu ya Roho Mtakatifu pasipo tofauti ya kutengana”. Sehemu hii ya ibada ya Misa Takatifu wakati wa adhimisho la Sherehe hii hutupatia kwa muhtasari maana ya Fumbo hili tunaloliadhimisha. Imani yetu katika Mungu mmoja si umoja wa nafsi bali ni Mungu mmoja katika nafsi tatu, yaani, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu.

Pengine inaweza kuwa ngumu kulielewa sawasawa fumbo hili lakini ufunuo wa Neno la Mungu katika Maandiko Matakatifu ni msaada wa kutosha kwetu. Lugha za kifalsafa zinaweza kuwa ngumu kwetu kuelewa baadhi ya misamiati yake mfano “nafsi”. Itoshe tu kuelewa kuwa Fumbo la Mungu ni uwepo ambao upo katika umoja na unaonekana katika nafsi tatu. Ni umoja usiogawanyika. Tunaweza kuuelewa mgawanyiko huu katika utendaji wao: kwamba Mungu Baba aliyetuumba, Mungu Mwana aliyetukomboa na Mungu Roho Mtakatifu anayetuuhisha, anayetutakatifuza na kutuongoza. Ufunuo huo wa Neno la Mungu ambao umetimizwa kwa Fumbo la Kristo umetufunulia kwa uwazi na kwa namna ya kueleweka juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Somo la Injili linatupatia msingi wa imani hii. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inatuelekeza wazi kuwa agizo la Kristo kwetu ni kubatizwa katika Utatu Mtakatifu. “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu”. Hili ni tangazo mahsusi na kiashirio cha imani yetu. Imani hiyo inajengeka katika huu Utatu Mtakatifu usiogawanyika. Kristo ambaye ni utimilifu na ufunuo wa fumbo la Mungu mara zote wakati wa maisha yake ya hadharani ametufundisha kwa namna mbalimbali juu ya Utatu Mtakatifu na zaidi katika namna ya utendaji wake. Hiyo ndiyo imani ambayo anatutuma kwenda kuitangaza leo hii, anatutuma kwenda kuwafanya mataifa yote kuiona na kuielewa imani hii. Kwa msingi huo, wajibu wetu sisi wabatizwa ni kuifunua haiba hii ya Mungu kwa watu katika namna ya utendaji wao.

Mungu ni Baba. “Kwa kumpa Mungu jina ‘Baba,’ lugha ya imani inaonesha hasa mambo mawili: Mungu ni mwanzo wa vitu vyote, na mwenye mamlaka makubwa, na pia mtunzaji wa watoto wake” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 239). Somo la kwanza linaufunua ukuu huu wa Mungu. Kitendo cha kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri kimeonesha jinsi ambavyo ana haiba hii ya kibaba ya kuitunza familia yake. Haiba hii pia inaufunua upendo wake mkubwa ambao kwa namna zuri unaelezeka katika haiba ya kimama. Hivyo, tunaweza pia kwa namna iliyofichika kumkiri Mungu katika umama. Kwa ujumla sehemu hii ya kwanza inaufunua ukuu wa Mungu katika taswira ya mzazi. Katika familia zetu tunawaweka wazazi wetu kama chanzo chetu, wanaotuongoza na pia wanaotupatia ulinzi.

Mungu kwetu anapokuwa Baba, sisi tunafanyika kuwa watoto wake. Somo la pili linatuambia kwamba: “Kila mtu anaongozwa na Roho wa Mungu, huyo ndiyo mtoto wa Mungu”. Hapa panatokea jambo jingine muhimu la umoja wa wana wa Mungu. Kwa kuwa Mungu ni mmoja, ambaye ni asili yetu, mlinzi wetu na tegemeo letu wote, sisi sote tunaunganishwa katika Yeye. Hapa tunamuona Mungu Roho Mtakatifu na tunaiona kazi yake: kutuongoza na kutufanya kuwa wana wa Mungu.

Roho Mtakatifu anatuongoza na kutufanya tuweze kulia, “Aba, yaani, Baba”. Tunapoutafari umoja huu wa Mungu usiogawanyika tunaelekezwa pia kuutafakari umoja wetu kama wanadamu, kwa kuwa tunaye Baba mmoja na hivyo sisi sote tumekuwa watoto wake. Hakuna asiyeumbwa na Yeye, asiyefadhiliwa na Yeye na asiyetunza na Yeye. Dhana hii itatupeleka katika kuimarisha undugu kati yetu na kuheshimu binadamu wote.

Mungu pia ni Mwana. Kristo, aliye Nafsi ya pili ya Mungu, amejifunua kwetu kama Mwana wa Mungu. “Jina ‘Mwana wa Mungu’ laonesha uhusiano wa pekee na wa milele kati ya Yesu Kristo na Mungu Baba yake: Yeye ndiye Mwana wa pekee wa Baba (Rej. Yoh 1:14, 18; 3:16, 18); na Yeye ni Mungu mwenyewe (Rej. Yoh 1:1)” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 454). Mwana wa Mungu ameutwaa ubinadamu wetu na kujifunua kwetu kama Mkombozi. Ukombozi wa Taifa la Israeli katika Somo la kwanza uliashiria ukombozi wa wanadamu wote ambao unatimilika kwa fumbo la Mwana wa Mungu kufanyika mwanadamu kwa ajili ya wokovu wetu. Hivi ni kama tunavyokiri katika Kanuni ya imani tukisema: “Ameshuka toka mbinguni, kwa ajili yetu sisi wanadamu, na kwa ajili ya wokovu wetu”.

Imani yetu kwa Mungu inapaswa kudhihishwa kwa namna tunavyoukumbatia upendo wake unaojifunua kwetu katika utendaji wake. Kwanza ni namna tunavyompokea Mungu kama chanzo chetu na uumbaji wote. Mali zetu, karama zetu na vyeo vyetu ni zawadi anayotupatia kusudi tumtumikie Yeye katika ndugu zetu. Vitendo vyoyote vya kibaguzi na kinyonyaji dhidi ya wenzetu na kuipora amana tuliyopewa na Mungu na kujipachika cheo cha umiliki. Ni kana kwamba tunayo haki miliki na mambo yetu. Mambo haya ndiyo chanzo cha mivurugano na machafuko mengi hapa duniani. Ili kustawisha haki na amani hapa duniani kwanza tunapaswa kumtambua kuwa Mungu ni Baba.

Pili ni namna tunavyompokea Mungu kuwa ni Mkombozi wetu. Ukombozi ambao uliletwa na Kristo ulijidhihirisha wazi katika kuustawisha ufalme wa Mungu ambao umefukuzwa na dhambi ya Mwanadamu. Ufalme wa Kristo ulinuia kutufanya tuishi katika ukweli, kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ulaghai na kupindisha ukweli kadiri ya Mungu unaendelea kuitafuna dunia. Huria ya kimaadili inatuingiza katika mgawanyiko mkubwa na maangamizi kwa utu wa mtu. Kila mmoja anajua vyote katika yote kwa kadiri ya ulimwengu wake. Hiki ndicho chanzo cha dhambi ya asili kwa mwanadamu kutaka kuwa kama Mungu. Tunapaswa kudhihirisha kuupokea ukombozi wa Mungu kwa kuisikiliza sauti ya Kristo inayoufunua ukweli wote, sauti ambayo tunaisikia kila siku katika Injili yake.

Tatu tunapaswa kumpokea Mungu kama kiongozi wetu. Katekisimu imetuambia kuwa Mungu ndiye anayetutunza. Katika Roho Mtakatifu tunayapata matunzo hayo kwa kutakatifuzwa, kuelekezwa njia na pia kuangaziwa. Sisi tunaompokea Roho Mtakatifu tunapaswa kuisikiliza daima sauti yake inayotusukuma kumuita Mungu ‘Aba, Baba’, na kwa njia hiyo kupata nafasi ya kuyaona yote katika muono wa Mungu na kuwa na ujasiri wa kuyashuhudia yote kadiri ya maongozi yake. Ni kuepuka kusikiliza sauti anuai ambazo zinatoka katika ulimwengu huu, sauti ambazo mara nyingi hutupatia elimu na ujasiri bandia. Sauti hizi bandia hutupeleka katika kuuharibu ubinadamu wetu.

Tuusifu Utatu Mtakatifu na umoja usiogawanyika. Hiyo ndiyo imani yetu tunayopaswa kuona fahati kuiungama. Tuidhihirishe imani hiyo kwa kuyapokea matendo yake makuu yanayodhihirishwa kwetu. Mungu ni Baba yetu, anatupenda na kutulinda; Yeye ni Mkombozi wetu anayetutoa katika njia ya upotovu na pia ni Kiongozi wetu anayetuangazia na kutufundisha yaliyo mapenzi yake kwetu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.