2018-05-23 14:29:00

Sakramenti ya Kipaimara inawawezesha waamini kuwa mashuhuda wa Kristo


Baada ya Katekesi kuhusu ushuhuda wa maisha ya Kikristo unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, Kipindi cha Mwaka wa Kanisa mara baada ya Sherehe ya Pentekoste, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 23 Mei 2018 wakati wa Katekesi yake ameanza kudadavua kuhusu Sakramenti ya Kipaimara, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa ili kuyatakatifuza malimwengu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanatajirishwa kwa mapaji ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuieneza na kuitetea imani kwa maneno  na matendo kama mashuhuda wa kweli wa Kristo.

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, Mkristo anapakwa Krisma ambayo inabubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe, yule ambaye Mwenyezi Mungu alimtia Mafuta kwa Roho Mtakatifu. Kumbe, Sakramenti ya Kipaimara inadokeza kwamba, inathibitisha Ubatizo na kuimarisha neema ya Ubatizo. Kwa mpako wa Krisma iliyochanganywa na manukato, na kuwekwa wakfu na Askofu, waamini wanampokea Roho Mtakatifu na hivyo kufafana na Kristo aliyetiwa Mafuta na Roho Mtakatifu. Hapa mwamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo anazaliwa katika maisha ya Kimungu na hivyo anapaswa kuishi na kutenda kama mwana mpendwa wa Mungu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Bila nguvu ya Roho Mtakatifu hakuna kinachoweza kufanyika, kama ilivyokuwa hata kwa maisha na utume  wa Yesu na ndivyo ilivyo hata kwa maisha na utume wa Kanisa. Wafuasi wa Kristo hata leo hii wako chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu.

Bikira Maria alipata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; Yesu alianza maisha yake ya hadhara baada ya kubatizwa Mtoni Yordani, mbingu zilipasuka, na Roho kama hua akashuka na kukaa juu yake. Yesu alipoingia  katika Sinagogi alitangaza na kushuhudia kwamba, “Roho wa Bwana yu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema. Kristo Yesu, Mpakwa wa Bwana alikuwa amejawa na Roho Mtakatifu. Huyu ndiye yule Roho Mtakatifu waliopewa Mitume, Siku ile ya Pasaka alipowatokea Mitume wake na kwa namna ya pekee kabisa, wakati wa Sherehe ya Pentekoste, wakajazwa na Roho Mtakatifu na kuanza kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa njia ya Sherehe ya Pentekoste, Kanisa liliweza kumpokea Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, kule Mtoni Yordani. Sherehe ya Pentekoste ni changamoto na ari ya kimisionari inayomtaka mwamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatakatifuza walimwengu na kushuhudia utukufu wa Mungu. Waamini kwa namna ya pekee kabisa, wanampokea Roho Mtakatifu wakati wa Sakramenti ya Kipaimara. Kwa hakika Roho Mtakatifu ni zawadi ya Mungu inayowaongoza waamini, ili waweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anazaliwa katika Maji na Roho Mtakatifu; kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, waamini wanampokea Roho Mtakatifu na kuwaweka wakfu ili kuweza kuwa ni mashuhuda wake; kwa kushiriki maisha na utume wa Kanisa. Ushuhuda amini, wenye mvuto na mashiko ni kielelezo makini cha mwamini kumpokea Roho Mtakatifu. Hii ni changamoto anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini kuwashirikisha wengine ujumbe wa Neno la Mungu. Ushuhuda wa maisha ya Kikristo ni kuishi na kutenda kadiri ya nguvu ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.