2018-05-23 16:01:00

Papa Francisko: Simameni kidete kutetea maisha, utu na heshima ya mtu


Ulimwengu mamboleo umegubikwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine pamoja na utamaduni wa kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kwa Kamati kuu tendaji ya Shirikisho la Ulaya lijulikanalo kama “One of Us”, ilipomtembelea na kuzungumza kwa faragha na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, matukio ya kifo laini “Eutanasia” yanaendelea kushika kasi sehemu mbali mbali za dunia na hata wakati mwingine, yanalindwa kwa sheria kinyume kabisa cha zawadi ya maisha, ambayo ndiyo haki msingi ya binadamu. Waathirika wakuu ni watoto ambao bado hawajazaliwa pamoja na wazee, ambao hawathaminiwi tena katika jamii. 

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika majadiliano kama haya, mara nyingi, “uzalendo wa kidiplomasia unamshinda”. Ndiyo maana anapenda kuwatia shime wajumbe wa Shirikisho la Ulaya, “One of Us” kusimama kidete na wala kutokubali kuyumbishwa, ili kweli utu, heshima na maisha ya kila binadamu yaweze kuheshimiwa na wagonjwa kupata tiba muafaka ya mahangaiko yao ya ndani. Huu ni wajibu wa kutambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano ya Mungu. Kwa upande wake, Carlo Casini, Muasisi na Rais wa heshima wa Shirikisho la Ulaya la “One of Us”, Bara la Ulaya halina budi kutambua usawa na utu wa kila binadamu, ili kuliwezesha Bara la Ulaya kusimikwa katika amani.

Itakumbukwa kwamba, Italia mwaka 2018, inafanya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Bunge la Italia lilipopitisha Sheria Namba 194 inayoruhusu vutendo vya utoaji mimba. Bwana Marcello Palmieri, mtaalamu bingwa wa maadiliviumbe anasema, vitendo vya utoaji mimba ni ukatili mkubwa unaooneshwa na binadamu ingawa maamuzi kama haya yanatetewa pia hata na Katiba, sheria na kanuni za nchi. Haki ya maisha ya mtu tangu anapotungwa mimba hadi pale anapofikwa na mauti ya kawaida, ni kielelezo cha thamani ya hali ya juu kabisa ambacho kamwe hakiwezi kulingamishwa na jambo lolote lile.

Afya ya binadamu; kiroho na kimwili haina budi kulidwa kwa dhati. Waamini wanapaswa kujenga na kudumisha dhamiri nyofu kwa kutambua kwamba, hapa ni mahali patakatifu ambamo Mwenyezi Mungu anapenda kuzungumza na waja wake. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wanawake wengi ambao wamekumbatia utamaduni wa kifo kwa kutoa mimba, lakini kwa upande mwingine madhara ya wanawake walitoa mimba hayazungumzwi hadharani. Vitendo vya utoaji mimba, vimerahisishwa sana kiasi kwamba, mwanamke ndiye anatekeseka sana na madhara ya utoaji mimba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.