2018-05-21 15:38:00

Shirika la Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa!


Wamisionari wa Roho Mtakatifu, ni Shirika lililoanzishwa na Padre Claude Poullart des Places, huko Ufaransa, tarehe 27 Mei 1703 katika Sherehe ya Pentekoste. Hiki kilikuwa ni kikundi cha Waseminari waliojiaminisha na kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu na kwa msaada wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa, hususan katika maeneo na mazingira tete na hatarishi; bila kusahau uinjishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Padre Joseph Shiyo, Mmisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu katika mahojiano na Vatican News anasema, karama ya Shirika ni uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima:kiroho na kimwili, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni Shirika ambalo linaendelea kujisadaka katika huduma ya Kanisa katika maeneo tete na hatarishi duniani, kama ilivyo huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, DRC na Sudan ya Kusini. Leo hii, Wamisionari wa Roho Mtakatifu wamenea katika nchi 63 duniani na Barani Afrika wanatekeleza utume wao katika nchi 28.

Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu wamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya elimu makini Barani Afrika; huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; pamoja na kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa, Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu linashirikiana kwa karibu sana na Shirika la Waconsolata, Wamisionari wa Afrika na  pamoja na baadhi ya Mashirika ya kitawa ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linatoa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kuunganisha  nguvu kama kielelezo makini cha ushuhuda katika huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.