2018-05-19 09:30:00

Maaskofu Katoliki Chile wameandika barua ya kung'atuka madarakani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Chile baada ya kusali, kutafakari na kupambanua kwa kina na mapana athari zilizosababishwa na nyanyaso za kijinsia nchini humo, kwa kauli moja, wameamua kumwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko kuomba, kung’atuka kutoka madarakani kama kielelezo makini cha uwajibikaji wao mbele ya Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Wanasubiri maamuzi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kila mmoja wao. Maaskofu wanasema, hija ya majadiliano katika ukweli na uwazi imekuwa ni msingi wa mageuzi yanayoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Chile, likiwa limeungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, linapenda kurejesha tena haki pamoja na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uponyaji wa madonda yaliyosababishwa na nyanyaso za kijinsia, ili kutoa ari na mwamko mpya wa utume wa kinabii katika Kanisa la Chile, daima, Kristo Yesu, akipewa kipaumbele cha kwanza. Ni matumaini ya Maaskofu Katoliki Chile kwamba, Uso wa Kristo Yesu, utang’ara tena nchini Chile na kwamba, wamedhamiria kuifuata njia hii. Baraza la Maaskofu Katoliki Chile, mwanzoni mwa tamko lao, wametumia fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko, kwa usikivu wake, uliowawezesha kukosoana kidugu. Wanapenda kuchukua fursa hii kuomba msamaha kwa waathirika, Kwa Baba Mtakatifu pamoja na familia ya Mungu nchini Chile katika ujumla wake kutokana na kashfa kubwa pamoja na kushindwa kutekeleza wajibu wao barabara.

Maaskofu wanawashukuru Askofu mkuu Charles Jude Scicluna pamoja na Monsinyo Jordi Bertomeu kwa majitoleo yao ya kitume, nguvu na juhudi walizofanya ili kuweza kuganga na kuponya madonda makubwa yaliyojitokeza ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wanawashukuru waathirika kwa moyo wa ujasiri na udumifu waliouonesha licha ya matatizo makubwa waliyokumbana nayo kama mtu binafsi, katika maisha ya kiroho, kijamii na kutoka kwa ndugu na jamaa, pengine hata ndani ya Kanisa lenyewe! Maaskofu wanawaomba msamaha na msaada wao ili waweze kusonga mbele katika mchakato wa uponyaji wa madonda na upyaishaji wa maisha na utume wao.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu, Francisko kuanzia tarehe 15-17 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile kwa faragha kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia, kwa kufuata mchakato wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kimekuwa ni kipindi cha kuchunguza dhamiri ili kupambananua sababu msingi zilizopelekea kuibuka kwa vitendo vya nyanyaso za kijinsia nchini humo. Baba Mtakatifu amewashirikisha Maaskofu taarifa iliyotolewa na uchunguzi uliofanywa na Askofu mkuu Charles Jude Scicluna hivi karibuni. Lengo kuu limekuwa ni kurejesha tena imani na matumaini ya watu wa Mungu kwa Kanisa nchini Chile.

Taarifa iliyotolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican inafafanua kwamba, Alhamisi, tarehe 17 Mei 2018 majira ya jioni, Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha kikao cha nne na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile! Maaskofu 34 wamehudhuria na kushiriki kikamilifu katika mkutano huu ambao umesimikwa katika umoja na udugu; ili kuweza kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa ari na moyo mkuu. Baada ya mkutano huu, Baba Mtakatifu amempatia kila Askofu barua ambamo anawashukuru kwa kukubali na kutikia mwaliko wake wa kufanya mang’amuzi ya pamoja dhidi ya matukio mabaya ambayo yameharibu umoja wa Kanisa pamoja na kudhohofisha utume wa Kanisa nchini Chile katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Katika mwanga wa matendo haya ya kusikitisha yaani kashfa ya nyanyaso za kijinsia; uchu wa madaraka na dhamiri, anasema Baba Mtakatifu wameweza kuzama zaidi na kuona uzito wa vitendo hivi na madhara yake hasa kwa waathirika.

Baadhi yao anasema, alipata bahati ya kuwaomba msamaha kwa niaba ya Kanisa na kwamba, Maaskofu katika utashi na umoja wao wamepania kurekebisha madhara yaliyojitokeza. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa majitoleo yao, ambayo kila mmoja wao, ameonesha ile nia ya kujiunga na kushirikiana na wote katika mchakato wa mabadiliko na suluhu ya kudumu, itakayoanza kutekelezwa hivi karibuni kwa kuzingatia malengo ya muda mfupi, muda wa kati na yale ya muda mrefu; mambo msingi katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka na umoja wa Kanisa unadumishwa. Mwishoni mwa barua yake, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, baada ya siku hizi za sala na tafakari, anapenda kuwaalika Maaskofu kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa la kinabii, linalotambua umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza katika huduma kwa Kristo Yesu anayeteseka kwa baa la njaa, kama mfungwa, mkimbizi na anayenyanyasika! Amewaomba Maaskofu Katoliki wa Chile kumkumbuka katika sala zao ili aweze kutekeleza vyema maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.