2018-05-18 16:22:00

Papa ametuma telegram ya salam za rambi rambi kufuatia kifo cha Kard. Hoyos


Baba Mtakatifu Francisko ametuma telegram kwa Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ya salama za rambi rambia kufuatia na kifo cha Kardinali Castrillon Hoyos.  Katika Telegram hiyo Baba Mtakatifu amesema, amepokea kwa masikitiko makubwa kuondokewa na mpendwa Kardinali Darío Castrillón Hoyos, na kwa maana hiyo anachukua nafasi hii kuonesha hisia zake za masikitiko na kuwatakia salam za rambi rambi Baraza la makardinali, familia na wote ambao wanaomboleza kwa kifo chake. Kadhalika anakumbuka kwa shukrani kuu kutokana na huduma yake aliyo ifanya kwa namna ya pekee kama Rais wa Baraza la Kipapa la Makleri na Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kanisa la Mungu. Anasali kwa Mungu ili  Bwana Mungu, kwa maombezi ya Bikira Maria aweze kumpokea kwa amani  na mwisho anawatumia baraka ya kitume wote wanaoshiriki uchungu wa kumpoteza mtumishi wa Injili.

Maisha ya Kardinali Darío Castrillón Hoyos na maombi kutoka kwa maaskofu wa Colombia. 
Kardinali Darío Castrillón Hoyos wa Colombia ameaga dunia mjini Roma usiku wa kuamkia 18 Mei 2018 akiwa na umri wa miaka 89 ambaye alikuwa Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Tume ya  Kanisa la Mungu. Alizaliwa mnamo tarehe 4 Julai 1929 huko Medellini nchini Colombia. Akapewa daraja Takatifu la Upadre manamo tarehe 26 Oktoba 1952 Kanisa la  Mtakatifu Roma wa Osos.  Baadaye yalifuata jajiundo yake mjini Roma katika Chuo Kikuu cha Urbaniano , mahali ambapo alipata shahada ya uzamivu wa Sheria za Kanisa. Baada ya kurudi nchini mwake alishika nyadhifa mbalimbali za huduma kichungaji hadi kuchaguliwa kuwa askofu mnamo tarehe 2 Juni 1971 kuwa msaidizi wa Askofu Álvarez Restrepo wa Jimbo la Pereira.

Baada ya Askofu wa jimbo kuaga dunia, yeye akaendelea na  nafasi hiyo kuanzia tarehe 1 Julai 1976.  Tangu 1983-1987 amekuwa katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Colombia na baadaye akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wake kwa miaka 8 kuanzia (1987-1991). Mnamo tarehe 16 Desemba 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu Mkuu wa Bucaramanga Colombia. Aliitwa mjini Vatican mnamo 15 Julai 1996 na kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la makleri hadi 2006. Akateuliwa kuwa Kardinali mnamo tarehe 21 Februari 1998 kwa kupewa Kanisa la Mtakatifu Maria Foro Taiano Roma. Tarehe 13 Aprili 2000 akateuliwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Tume ya Kanisa la Mungu hadi kustaafu kwake 8 Julai 2009.
 
Baraza la Maaskofu wa Colombia wanaungana pamoja na waamini wote kusali ili roho yake ipumzike kwa amani. Na Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Colombia Askofu Mkuu Oscar Urbina Ortega anasema, Kristo Mfufuka ampokee katika maisha ya milele mtumishi wake aliye jitoa kwa ukarimu kulitumikia Kanisa kama mchungaji mwema kwa watu wa Mungu. 

Wakati huo huo, taarifa kutoka kwa Monsinyo Guido Marini, Mshehereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican, ametoa ratiba ya mazishi ya Kardinali Hoyos itakayo ongozwa na Kardinali Angelo Sondano, Dekano wa Makardinali ambapo ratiba elekezi ya mazishi itakuwa ni siku ya Jumamosi tarehe 19 Mei 2018 saa 8.30 mchana masaa ya Ulaya katika Altare Kuu ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Misa itaudhuriwa na makardinali, maaskofu na waamini, ambapo mara baada ya misa, Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha na liturujia ya mazishi hayo na kubariki.

Sr Angela Rwezaula 
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.