2018-05-18 14:32:00

Balozi Possi: Watanzania dumisheni: amani, umoja, ukweli na uadilifu


Watanzania wanapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja, udugu, Amani, ukweli na uzalendo unaofumbatwa katika kanuni ya dhahabu, yaani kila mtu amtendee jirani yake, yale anayotaka kutendewa na wengine na kwamba, kila mtanzania ajivunie utanzania wake! Viongozi wa kidini wasaidie kujenga jamii inayosimikwa katika kanuni maadili na utu wema, jamii yenye hofu ya Mungu na ambayo inaongozwa na dhamiri nyofu katika kufikiri, kuamua na kutenda! 

Haya ni maneno mazito yaliyotolewa na Dr. Abdallah Saleh Possi, Balozi  mpya wa Tanzania mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 17 Mei 2018 baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, jioni alipata nafasi ya kukutana na watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, waliokuwa wamekusanyika kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kushuhudia Padre Celestine Richard Nyanda, a.k.a “Sauti ya kinabii” akipambana kiume kutetea kazi yake ya shahada ya uzamivu katika sheria kanuni za Kanisa.

Dr. Abdallah Saleh Possi anayewakilisha pia Tanzania katika maeneo 10 licha ya Ujerumani na Vatican amewakumbusha wakleri na watawa kwamba, wao kimsingi, wanapaswa kuhudumiwa na Ubalozi wa Tanzania mjini Vatican, kadiri ya kanuni za kidiplomasia, lakini mara nyingi wakleri na watawa hawa wamekuwa wakipata huduma yao kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Sera na mikakati ya sasa anasema Dr. Possi ni kujenga na kuimarisha “Diaspora ya Tanzania” katika maeneo yote anayowakilisha. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa watanzania kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara, kutoa maoni na ushauri ili kuboresha huduma kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Anaendelea kufafanua kwamba, kuna uhusiano na ushirikiano mkubwa kati ya taasisi za kidini na serikali nchini Tanzania katika huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu pamoja na mapambano dhidi ya umaskini.

Dr. Possi anasema, umaskini wa Bara la Afrika unachangiwa na mambo ambayo yako nje ya uwezo wa Bara la Afrika, lakini, mambo mengi yako ndani ya uwezo wa Waafrika wenyewe! Ufisadi, rushwa na wizi wa mali ya umma ni matokeo ya uchoyo, ubinafsi, kukosekana kwa hofu ya Mungu na upendo kwa jirani. Ni dhamana nyeti kwa viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanasaidia kujenga na kufunda dhamiri nyofu, kanuni maadili na utu wema.

Anakaza kusema, anajivunia kuwa Mtanzania kwani hii ni nchi ya pekee kabisa Barani Afrika, iliyobahatika kukita mizizi yake katika: umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa unaovuka: udini, ukabila na itikadi za kisiasa. Hii ni jumuiya inayopaswa kuishi kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi. Dhamana na wajibu wa viongozi wa kidini ni kusaidia mchakato wa kujenga na kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wasaidie kuwafafanulia waamini wao dhamana na wajibu wao katika mustakabali wa ujenzi wa nchi yao sanjari na kukuza tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu na kusaidia kuleta maendeleo endelevu ya binadamu. Watanzania wathaminiane na kuheshimiana; walinde na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kutambua kwamba, amani ni chachu ya maendeleo. Amani ikitoweka, watu wengi watateseka! Kumbe, ni dhamana ya viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha amani inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayoongozwa na kanuni ya dhahabu; kwa kutafuta na kudumisha kilicho chema na kizuri; ili kujenga taifa lenye ustawi na maendeleo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.