2018-05-17 08:09:00

Umuhimu wa majadiliano ya kidini katika kukuza utu, haki na amani!


Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani ni mchakato muhimu sana katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; yanapania pamoja na mambo mengine, kuendeleza uhuru wa kuabudu, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wa dini mbali mbali wanakabiliwa na changamoto kuu tatu: Mosi, Utambulisho wa dini yao; nani ni Mungu wao na ushuhuda wa maisha mintarafu kile wanacho kiamini katika maisha.

Pili, ni changamoto ya kuheshimu watu wenye imani tofauti kwa kutambua kwamba, hawa si adui bali ni wanandani wa hija ya maisha kuelekea katika ukweli. Tatu, ni changamoto ya ukweli katika imani wanayoungama na kuishuhudia. Yote haya yakizingatiwa kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, hakuna sababu ya vita vya kidini, nyanyaso wala dhuluma kwa misingi ya kiimani kama inavyoshuhudiwa kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia.

Kumbe, majadiliano ya kidini ni fursa ya kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayoheshimu tofauti-msingi kama utajiri na changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu kati ya watu wa Mungu. Majadiliano ya kidini hayana budi kusimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kutambua na kuthamini utambulisho wa maisha ya kiroho sanjari na kudumisha katekesi makini ya kila mwamini katika dini yake bila ya kutaka kufanya wongofu wa shuruti.

Majadiliano ya kidini ni fursa muhimu sana kwa waamini kuweza kutangaza na kushuhudia imani yao; kwa kuheshimu na kuthamini uwepo wa dini za watu wengine ndani ya jamii na kuwaelekeza katika hija inayowapeleka kwa Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wote. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini hivi karibuni, limehitimisha “mazungumzo awamu ya tano ya majadiliano ya kidini” huko Ammani, nchini Yordan kwa kushirikiana na Taasisi ya Kifalme ya Majadiliano ya Kiimani, “RIIFS” na kwamba, Mfalme El Hassan Bin Talal ameratibu majadiliano haya. Askofu Miguel Ayuso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini alimwakilisha Kardinali Jean Louis Tauran.

Majadiliano haya yameongozwa na kauli mbiu “Dini; utu wa maisha: Changamoto: kutoka katika mitazamo ya Kiislam na Kikristo. Wawezeshaji wakuu katika majadiliano haya walikuwa ni Professa Abdel Jabbar Al Refae, Dr. Youssef Kamal El-Hage; Prof. Wajih Kanso; Monsinyo Khaled Akasheh; Monsinyo Bernard Munono, Prof. Mohammad Ali Azar Shab pamoja na wageni waalikwa kama vile Mufti mkuu Husein Kavazovic, Dr. Paola Bernardini pamoja na Prof. Hichem Grissa.

Majadiliano haya yamefanyika katika mazingira ya uelewano na urafiki mkubwa; ukweli na uwazi. Imekuwa ni fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu tema hii tete na mwishoni, wametoa tamko la pamoja kwa kusisitiza kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Binadamu ni kilele cha kazi ya uumbaji, amekirimiwa utu, haki na dhamana katika maisha yake. Hii ndiyo maana kila mtu anapaswa kuheshimiwa, kupendwa na kukuzwa utu na heshima yake. Kuna uhusiano mkubwa katika mbinu mkakati wa kuheshimu utu wa binadamu, haki zake msingi pamoja na mafungamano ya kijamii. Kila binadamu anavionjo, tunu na mawazo yake yanayopaswa kuheshimiwa.

Wajumbe wamegusia changamoto na wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji; waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; makundi ya watu yanayohitaji huduma ya pekee, ili kudumisha maisha, utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau maana ya ndani kabisa ya mahangaiko ya mwanadamu. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuelimishwa umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; maisha, utu na heshima ya binadamu.

Vijana wafundishwe na kurithishwa kanuni maadili na utu wema na kwamba, wanapaswa kuzingatia masomo kama ufunguo wa maisha yao ya baadaye. Wajumbe wameushuruku uongozi wa Taasisi ya Kifalme ya Majadiliano ya Kiimani, “RIIFS” chini ya Dr. Majeda Omar pamoja na wafanyakazi wote. Wajumbe wa majadiliano haya wamekubaliana kimsingi kuendeleza majadiliano haya. Chuo Kikuu cha Ez-Zitouna, Tunisia na Kituo cha Majadiliano na Vitendo, Pakistan navyo vimetia sahihi kuendeleza ushirikiano huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.