2018-05-15 08:56:00

Wanawake nchini DRC wanajifunga kibwebwe kupambana na hali yao!


Wanawake wanapaswa kujituma, kujiamini na kujisadaka katika maisha yao, ili waweze kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa kutambua kwamba, wanayo dhamana kubwa na nyeti katika maisha na utume wa familia na jamii katika ujumla wake. Wanawake wakiisha kujiamini wataweza kukuza na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Kanisa liwe na ujasiri wa kupambana na nyanyaso, dhuluma na uonevu wanaokumbana nao wanawake katika maisha na utume wao! Umefika wakati kwa Mama Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wanawake wanaoteseka kutokana na mifumo mbali mbali ya ukandamizaji: katika familia, maeneo ya kazi na hata katika maisha ya hadhara. Umaskini wa wanawake Barani Afrika ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuwakoa kutoka katika utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima yao, kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi, ili kuweza kupambana na hali pamoja na mazingira yao.

Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco limebuni na kugharimia wa kilimo kwa ajili ya wanawake wanaoishi katika kitongoji cha Ngafula, Jimbo kuu la Kinshasa, nchini DRC, ili kuwawezesha wanawake kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na fedha kwa ajili ya mahitaji yao pamoja na familia zao. Hii ni sehemu ambayo ina uhaba mkubwa wa maji safi na salama; wala haina umeme! Kumbe, juhudi za kuwajengea wanawake uwezo wa kuzalisha mazao ya chakula na biashara zinaanza kuzaa matunda, kwa wanawake kutoka katika familia mbali mbali kuwa na uwezo wa kiuchumi. Kwa sasa wanawake hao wameanza kujipanga ili kupanua kilimo kitakachowawezesha kupata mazao mengi na hivyo kujiongezea kipato.

Wanawake kutoka katika Parokia ya Don Bosco wanasema, fedha itakatopatikana kwanza itatumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya kifamilia, elimu kwa watoto wao pamoja na huduma kwa jamii inayowazunguka. Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco kwanza limeamua kutoa elimu ya kilimo bora na ufugaji wa kisasa; kwa kuwapatia wanawake zana na pembejeo za kilimo na ufugaji wa kisasa. Kuna mpango wa kujenga bwawa litakalotumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Mradi huu pamoja na mambo mengine, unapania kuzalisha mboga mboga ili kutosheleza mahitaji ya soko la ndani. Lakini, ili kuweza kufanikisha yote haya, wanawake hawana budi kujituma, kujiamini na kujisadaka kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu ya familia na jamii zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.