2018-05-15 10:30:00

Askofu mkuu Rugambwa asema, Askofu mpya ni alama ya upendo wa Mungu


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amehitimisha safari ya kichungaji iliyomwezesha kutembelea Namibia na Botswana, ili kujifunza zaidi maisha na utume wa Makanisa mahalia; kuangalia: matatizo, changamoto na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Imekuwa ni fursa kuwatia shime wamisionari pamoja na mihimili yote ya uinjilishaji kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha furaha ya Injili!

Akiwa nchini Namibia, Askofu mkuu Rugambwa, hapo tarehe 5 Mei 2018 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na kumweka wakfu Askofu Willem Christiaans, OSFS, wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop, ili aweze kutoa huduma patakatifu pa Mungu: kwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kama kilele cha huduma takatifu. Kwa namna hii, Askofu hushika nafasi ya Kristo mwenyewe, aliye mwalimu, mchungaji na kuhani na kwamba, anatenda kazi hii kwa nafsi ya Kristo. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Maaskofu kutoka ndani na nje ya Namibia kuonesha urika wa daraja ya uaskofu.

Askofu mkuu Protase Rugambwa katika mahubiri yake amesema, uteuzi na ahataimaye, kuwekwa wakfu kwa Askofu Willem Christiaans ni alama hai ya upendo wa Mungu na utimilifu wa ahadi yake kwa waja wake kwamba, atawapa wachungaji waupendezao moyo wake, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu. Huyu ndiye mchungaji ambaye Mwenyezi Mungu katika ukuu, wema na huruma yake, ameijalia familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Keetmanshoop. Kama ilivyo kwa kila Askofu, kama wakili wa Kristo, ana kazi ya kichungaji kwa Kanisa mahalia ambalo ameaminishwa, lakini papo hapo, kiurika, pamoja na ndugu zake katika uaskofu, anajishughulisha kwa ajili ya Makanisa yote.

Askofu mkuu Rugambwa, mwanzoni mwa Ibada ya Misa Takatifu, amewapatia watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Keetmanshoop salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Amewashuruku viongozi na mihimili yote ya uinjilishaji, vyama na mashirika ya kitume pamoja na waamini walei, kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo ndani na nje ya Jimbo lao.

Askofu mkuu Rugambwa, amemsihi Askofu Willem Christiaans kuonesha na kushuhudia upendo wake kwa Kristo Yesu, daima akiomba neema, ya kuendelea kudumu katika pendo hili, ili aweze kumpenda zaidi kuliko mambo mengine yote! Upendo wa dhati kwa Kristo Yesu, unamwilishwa katika huduma makini kwa ajili ya wokovu wa familia ya Mungu. Lakini, ubora na ufanisi wa huduma hii, unategemea kwa kiasi kikubwa mahusiano na mafungamano kati ya Askofu mwenyewe na Kristo Yesu, ambaye anamwakilisha kama wakili mwaminifu. Kama kiongozi mkuu wa watu wa Mungu Jimboni mwake, atapaswa pia kuwapenda na kuwathamini waamini wake! Askofu aoneshe upendo mkubwa kwa wakleri ambao wanashirikishana utume wao kwa Kristo! Awatambue na kuwaona kama watoto na ndugu zake katika Kristo Yesu; ajali na kuthamini mchango wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Akuze na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini, ili upendo wa Kristo uweze kung’aa kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaotolewa na Askofu.

Kimsingi, kama Askofu aguswe na mahangaiko ya watu wote bila kuangalia umri, nafasi yao katika jamii, utaifa, wazawa au wageni! Wote hawa waonje huruma na upendo wa Kristo unaobubujika kutoka kwa Askofu mahalia! Wajibu wake mkuu utakuwa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa; pamoja na kuwaongoza watu wa Mungu katika mchakato wa kutafuta na kuambata: haki, amani na maridhiano kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wa Mungu. Kwa namna ya pekee kabisa, kama Askofu anapaswa kuonesha upendeleo kwa maskini, wanaoteseka na wanyonge katika jamii. Atambue dhamana na wajibu wa Askofu, daima ajitahidi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Awe mwepesi kujiweka chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu ambaye amemweka wakfu kwa njia ya Krisma ya Wokovu ili kwa njia yake pamoja naye na ndani yake, aweze kuwa ni mchungaji mwema wa kundi la Kristo!

Itakumbukwa kwamba, Askofu Willem Christiaans, OSFS, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop, lililoko nchini Namibia. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Willem Christiaans alikuwa ni Msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop. Alizaliwa tarehe 12 Februari 1961 huko Gabis, Karasburg, Jimbo Katoliki la Keetmanshoop. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa akaweka nadhiri zake za daima tarehe 23 Januari 1988 na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre 10 Desemba 1988. Katika maisha na utume wake kama Padre, Askofu Willem Christiaans amewahi pia kuwa ni mkurugenzi wa wanafunzi wanaojiandaa kuingia hatua ya Unovisi Shirikani kwake; Mkurugenzi wa wasomi wa Shirika, Mkuu wa Shirika Kikanda tangu mwaka 1993 hadi mwaka 2005, kwa vipindi vitatu mfululizo. Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2013 amekuwa Paroko, Makamu wa Askofu, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa na tarehe 26 Julai 2017 akateuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop, lililoko nchini Namibia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.