2018-05-10 15:23:00

Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni!


Siku arobaini baada ya Ufufuko wa Kristo Kanisa huadhimisha Sherehe ya kupaa Bwana mbinguni. Sherehe hii huadhimishwa siku ya Alhamisi baada ya Dominika ya 6 ya Pasaka na mara nyingi kutokana na changamoto za kichungaji husogezwa mbele na kuadhimishwa katika Dominika ya 7 ya Pasaka na hivyo kutoa fursa kwa waamini wengi kuisheherekea siku hii. Katika sala ya mwanzo ya sherehe ya leo tumesema: “huko alikotutangulia yeye kichwa chetu, ndiko tunakoamini kufika sisi tulio mwili wake”. Tunaadhimisha tukio la furaha sana katika historia ya ubinadamu wetu kwani mbingu na dunia vinaungana tena. Yeye aliutwaa ubinadamu wetu anakuwa mwakilishi wetu huko juu mbinguni. Ubinadamu wetu uliokombolewa, ulio katika hali ya utukufu wa ufufuko sasa unakaa pamoja na Mungu huko juu mbinguni.

Tukio la kupaa Bwana linaashiria hitimisho la utume wake aliotumwa na Baba na kufungua mlango kwetu sisi wafuasi wake kuanza kuuendeleza, tukianzia na mitume wakati wa Kanisa la mwanzo kabisa hadi kwetu sisi tunaomfuasa leo hii. Utume huo ambao Kristo aliutamka waziwazi tangu mwanzo wa utume wake wa hadharani ulikuwa ni kumkomboa mwanadamu. Kristo alianza kwa kusema: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema, amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” (Lk 4:18 – 19). Hivyo Kristo asemapo “nanyi mtakuwa mashahidi wangu” anatualika kuuendeleza uwepo wake katikati ya maskini, wafungwa na vipofu katika jamii yetu ya leo kwa kuwatangazia habari njema.

Tangu kupaa kwake mbinguni kazi hii ya Kristo imeendelezwa na ametuelekeza kuidumisha kazi hii siku zote kwani yupo nasi katika utume huo. Ni Yeye ambaye anatenda ndani mwetu kupitia Roho wake Mtakatifu. Yesu aliwaambia mitume: “lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu”. Kabla ya kuteswa kwake wakati wa mahusia yake ya mwisho wakiwa katika Karamu ya Mwisho Kristo aliwaeleza wazi mitume nafasi ya Roho Mtakatifu: Ni yeye anayekumbusha na kufundisha kile ambacho aliwafundisha (Rej Yoh 14:26), ni yeye atakayemshuhudia Kristo (Rej Yoh 15:26) na atanena si kwa shauri lake bali shauri la Baba na pia yale yajayo atatoa habari yake (Rej Yoh 16:13). Hivyo Roho Mtakatifu ni nguvu yetu wakati wa madhulumu, tulizo letu wakati wa taabu na tegemeo letu katika magumu. Yeye ni mwalimu wetu kwani hutufundisha na kutuelekeza tupaswayo kuyafanya na pia ni nguvu yetu kwa kuwa anatupatia ujasiri wa kusonga mbele na kumshuhudia Mungu.

Ni dokezo muhimu katika kuupokea utume huu wa ukombozi wa mwanadamu kuwa umetoka kwa Mungu. Ni Yeye ambaye anatumia vipawa vyetu mbalimbali ili kuukomboa ubinadamu wetu. Ni taadhari kuepuka kutawaliwa na kiburi na majivuno ya kujiona kuwa tunajiwezesha. Mwanadamu anayejikinai katika uwezo wake na kumuacha Mwenyezi Mungu huangukia mara zote katika mafarakano na wenzake na mwisho ni kupoteza upendo na kuvunjika kwa undugu. Katika mantiki ya kawaida mwanadamu anayetengana na mpango wa Mungu atafanya yote kadiri aonavyo yeye; akiwa ameathiriwa na mazingira yake, jamii anayoishi, historia yake na mengineyo mengi ni wazi mmoja atajikuta anajitengenezea utaratibu binafsi unaokinzana na wengine. Hivyo kila mmoja akifanya yake basi zao lake ni mafarakano.

Jamii yetu ya leo inabidii sana kutafuta uhuru wa mwanadamu bila kujali ukweli. Namna hii imeendelea kuharibu haiba ya mwanadamu. Hivi karibuni Raisi ya Jamhuri ya Italia Sergio Mattarella alisema: “ukweli hauwezi kuepukika katika uhuru wa kweli”. Kwa namna ya pekee maneno hayo yanaendana na ujumbe wa Baba Mtakatifu katika siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yenye kichwa cha habari: “Ukweli utawaweka huru: Habari za kughushi na uandishi wa habari wa amani”. Tasnia ya habari inao mchango mkubwa sana kuueneza ukweli na kuufanya utume wa Kristo kuendelea katika ulimwengu wa leo. Lakini katika hali kinzani leo hii tunashuhudia habari za kughushi ambazo kwa sehemu kubwa zinakinzana na juhudi ya kumkomboa mwamnadamu. Wengi wa waandishi husukumwa na ubinafsi wao uwe wa kiuchumi, kijamii au kisiasa bila kujali kuharibu haiba ya watu wengine. Baba Mtakatifu anatukumbusha kuepukana na habari za namna hiyo na kuandika ukweli ambao utaleta amani na ukombozi kwa mwanadamu.

“Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe”. Habari njema ya wokovu sharti iwafikie watu wote. Uwepo wa Kanisa unaonekana katika huduma hiyo. Habari njema ni lazima kuwafikia watu wote na hivyo tukitafakari uhalisia wa ulimwengu wetu, tukiangalia namna ambavyo watu wengi bado wanahangaika wakitafuta ukombozi, bado tunauona uhitaji na udumifu wa utume huu. Huduma hii haiwezi kukoma kwani kila mara huibuka madhulumu dhidi ya ubinadamu. Ukweli huu husababishwa na udhaifu wa mwanadamu ambaye mara zote anaposhawishiwa na shetani humsababishia mwanadamu mwingine kusongwa na maswahibu ya maisha. Matendo mengi maovu, mathalani rushwa, ukahaba, vita, magomvi, misigano katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na hata kijamii ni ishara tosha ya ukengeufu wa mwanadamu na matokeo yake ni mateso, mahangaiko na huzuni kwa wengine. Katika muktadha huu tunaona udumifu na umuhimu wa habari njema wakati wote.

Sisi wabatizwa tumepokea cheo hiki kikubwa na wajibu wa kuutangazia umma hadhi hiyo. Maisha yetu ya kikristo yanapaswa kuendeleza utume wa Kristo. Tunaalikwa leo kuwa mashuhuda, yaani kwenda kuufanya ubinadamu ukutane na Kristo. Katika ngazi ya familia tunatumwa kumwonesha Kristo kwa wanafamilia wote. Asiwepo mmoja ambaye amesambaratishwa na madhulumu ya dunia hii na kukosa amani hata ndani ya familia. Baba kama kiongozi wa familia aiongoze vyema familia yake bila ubinafsi wala mabavu; mama kama mlezi wa familia azitekeleze vema tunu zake za kimama; watoto wajifunze ndani ya familia kuwa ndugu.

Utii, upendo na undugu utokao ndani ya familia uchanue hadi katika maisha ya kawaida ya jamii na kwa njia hiyo ubinadamu utaokolewa kwani sote tutaishi kama ndugu. Na huo ndiyo utume wetu tunaotumwa kuushuhudia, utume ambao utaendeleza uwepo wa Kristo katikati yetu. Hivyo tusisite bali twendeni tukiwa na nguvu na matumaini. Hii ni kwa faida yetu na ndugu zetu wote na huu ni mradi wa mwenyezi Mungu mwenyewe na hivyo Yeye ndiye atakayetuwezesha. Twendeni tukaujenge ufalme wa Mungu kusudi tuanze kuuonja tungalipo hapa duniani na mwishoni tuungane na Kristo huko mbinguni alipotutangulia kwani ametuambia kuwa anakwenda kutuandalia makao.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.