2018-05-10 13:21:00

Papa: Utamaduni wa maisha mapya unasimikwa katika sheria ya udugu!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza hija yake ya kichungaji Nomadelfia, Alhamisi, tarehe 10 Mei 2018 kwa kusali kwenye kaburi la Don Zeno Saltini, muasisi wa Jumuiya ya Kikundi cha Familia kunako mwaka 1947, akakutana na kuzungumza kwa faragha na kikundi hiki na baadaye akapata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Nomadelfia waliokuwa wamefurika asubuhi na mapema ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu. Jumuiya ya Nomadelfia ni ukweli wa kinabii unaopania kujenga utamaduni mpya unaomwilisha Injili kama chemchemi ya wema na uzuri.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amekazia kwa namna ya pekee, sheria ya udugu katika maisha ya kijumuiya mintarafu maisha ya Jumuiya ya Wakristo wa Kanisa la mwanzo; huduma ya upendo kwa wazee na ushuhuda unaomwilishwa katika tunu msingi za maisha ya kifamilia. Baba Mtakatifu anasema, ameamua kuja kuwatembelea, ili kuwatia shime kuendeleza Jumuiya iliyoanzishwa na Don Zeno Saltini kama sehemu ya kumwilisha Injili ya Kristo kama njia ya maisha yanayofumbatwa katika wema na uzuri.

Don Zeno alijitaabisha usiku na mchana ili kuandaa mazingira, akapanda mbegu ya Injili na sasa matunda ya utamaduni wa maisha mapya yanaanza kuonekana. Ni kiongozi aliyejitahidi kusoma alama za nyakati, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; akakumbana na magumu pamoja na changamoto za maisha ya kila siku, lakini yote haya yakawa ni nguvu ya Injili iliyopyaisha maisha ya watu wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Don Zeno alikita maisha ya Jumuiya ya Nomadelfia katika sheria ya udugu kama ilivyokuwa kwa Jumuiya ya Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliokuwa na moyo na roho moja. Huu ndio mtindo wa maisha unaopaswa kuendelezwa, kwa kujiaminisha katika nguvu ya Injili na Roho Mtakatifu kama njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko! Ni Jumuiya ambayo imeweza kuwatangazia watoto maskini, yatima na wagonjwa Injili ya upendo, lugha ambayo imeingia na kuzama katika maisha yao.

Jumuiya hii ikashinda kishawishi cha upweke hasi na kuanza kujikita katika umoja na mshikamano wa familia mbali mbali, ambamo wanajumuiya wote wanajisikia kuwa ndugu wamoja katika imani. Kwa njia hii, wakawa pia ni ndugu zake Kristo Yesu, kwa kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu. Kama alivyosema Kristo Yesu mwenyewe, hawa ndio mama na ndugu zake Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasema, hii ni Jumuiya inayosimikwa katika udugu na maisha ya kifamilia yanayowawezesha wanajumuiya wote kufahamiana hata kwa majina na kuthaminiana kama ndugu wamoja.

Jumuiya ya Nomadelfia ni alama ya unabii inayoonesha utu wa wananchi wa Nomadelfia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya upendo kwa wazee na wagonjwa wanaokabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Hawa ni watu ambao daima wameendelea kupata huduma katika familia, kama kielelezo makini cha upendo wa kidugu unaomwilisha Injili ya upendo katika uhalisia wa maisha ya watu. Don Zeno Saltini alipenda kuona Jumuiya iliyokua inazingatia mambo msingi katika maisha na miundo mbinu yake; akatangaza na kushuhudia furaha ya Injili ya Kristo, msingi wa furaha na utulivu wa maisha ya Jumuiya ya Nomadelfia yanayobubujika kutoka katika Injili. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa ushuhuda ambao ataendelea kuuhifadhi katika sakafu ya maisha na utume wake kwa njia ya sala. Ataendelea kukumbuka nyuso za familia hii kubwa iliyopigwa chapa ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.