2018-05-09 16:03:00

Loppiano ni daraja linalowakutanisha watu wa dini, imani na tamaduni


Loppiano ni Makao Makuu ya Chama cha Kitume cha Wafokolari, mahali ambapo watu wa dini na makanisa mbali mbali wanaweza kukutana ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anakazia sana mchakato wa majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika kukuza na kudumisha amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi na kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani!

Majadiliano ya kidini yanapania pamoja na mambo mengine kuendeleza uhuru wa kuabudu, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu pamoja na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha Kitume cha Wafokolari anasema, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 10 Mei 2018 anawatembea ili kushuhudia jinsi furaha ya Injili na Upendo inavyomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wanachama wake.

Kwa mara ya kwanza, Khalifa wa Mtakatifu Petro anatembelea Loppiano, ingawa daima Mababa Watakatifu wamekuwa wakiwatia shime kwa ujumbe kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa kuzindua Kanisa la Bikira Maria, Mama wa Mungu, “Theotokos”. Chama hiki kilianzishwa kunako mwaka 1964 na kimekuwa ni maabara ya umoja na udugu, unaowaunganisha watu 850 kutoka katika mataifa 65. Hiki ni kitovu cha: udugu, upendo, ukarimu na majadiliano katika uhalisia wa maisha ya watu yanayofumbatwa katika huduma!

Loppiano umekuwa ni daraja la watu kutoka mataifa, tamaduni na dini mbali mbali kukutana. Ni mahali pa malezi na majiundo ya kiutu; mahali pa udugu na urafiki anasema Luigino Bruni, mwanachama wa Chama cha Kitume cha Wafokolari. Loppiano ni kitovu cha karama, maisha na utume wa Chiara Lubich. Hapa ni mahali ambapo tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Hapa ni mahali ambapo waamini walei kwa njia ya ushuhuda wa maisha, wanajitahidi kuyatakatifuza malimwengu. Ni mahali pa sala, tafakari, maisha na kazi. Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko mahali hapa ni chemchemi ya furaha, matumaini na mapendo hasa wa wagonjwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Loppiano ni kitovu cha Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.