2018-05-08 15:33:00

Rais Mattarella:Mazungumzo ya muungano wa vyama Italia yashindikana!


Mazungumzo ya muungano wa vyama nchini Italia yameshindikana, hivyo kuiacha nchi ikitakiwa kufanya uchaguzi mpya au kuwa na serikali ya mpito hadi mwishoni mwa mwaka huu. Hayo ni kwa mujbu wa Rais Sergio Mattarella jioni ya tarehe 7 Mei 2018 akiwa anatarajiwa na taifa zima kutoa kauli yake ya mwisho kuhusiana na suala hili ambalo limetingisha vikali nchi ya Italia.

Rais Mattarella, amesema mazungumzo na wakuu wa vyama ndiyo yalikuwa tegemeo la kulifikisha taifa katika makubaliano kufuatia vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu mwezi machi mwaka huu kutofanikiwa kupata ushindi. Rais Matarella amethibitisha kuwa hadi sasa, hakuna chama chochote binafsi kilichopata kura za kukiwezesha ushindi kama chama. Hata hivyo vyama viwili maarufu vilijulikanavyo “Nyota tano” “Lega”, ndivyo vinavyochuana kwa karibu sana pamoja na kwamba hawakubali kukaa pamoja kujenga mshikamano.

Mazungumzo yaliyoshindikana yalikuwa na lengo la kuunda serikali ya muungano, japo kuwa chama kikuu  kilipinga hatua hiyo ya kuungana na chama kingine kile cha kulia (Destra au kushoto Sinistra). Rais Matterella akizungumza siku ya Jumatatu jioni  kwa njia ya televisheni, ametoa  rai kwa viongozi wa vyama vyote kuunga mkono serikali huru isiyoegemea upande wowote, hasa baada ya kushindikana kuundwa kwa serikali ya muungano wa vyama na kusisitiza kwamba hawawawezi kuendelea kusubiri kukaa bila ya kuwa na serikali.

Aidha Bwana Mattarella ameongeza kusema, serikali hiyo hiyo isiyofungamana na upande wowote wa vyama, ndiyo iwe na jukumu la kuandaa bajeti ya mwaka 2019 ili kuliepusha taifa hilo kushuka kiuchumi. Serikali hiyo ya mpito itaendesha taifa hilo hadi mwishoni mwa mwaka na baadaye kufikia ukomo wake baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2019. Hadi sasa si chama cha Nyota tano “Cinque stelle”  na “Lega” ambavyo vimeonesha kuunga mkono mawazo hayo.

Sr Angela Rwezaula
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.