2018-05-08 13:26:00

Papa Francisko: Tushikamane kupambana na utumwa mamboleo duniani!


Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara, matumizi na usambazaji haramu wa dawa za kulevya. Kashfa hii imeanza kuzoeleka kati ya watu, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni jambo la kawaida katika maisha. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo na mifumo yake yote, inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwani huu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu na ni janga la kimataifa!

Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa video kwa washiriki wa Jukwaa la Pili la Kimataifa Dhidi ya Utumwa Mamboleo linaloongozwa na kauli mbiu “Matatizo ya zamani katika ulimwengu mamboleo”, ambalo limefungulia nchini Argentina kuanzia tarehe 5-8 Mei 2018. Jukwaa hili limeandaliwa na Jimbo kuu la Buenos Aires, Kanisa la Kiorthodox kwa kushirikiana na Taasisi ya Athenagoras ya Backley, kutoka California, nchini Marekani. Viongozi wakuu wa Makanisa kama Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kianglikani wanashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya mifumo ya utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anakaza kusema, mifumo ya utumwa mamboleo ina mizizi yake katika historia na maisha ya binadamu na kila wakati inajipyaisha na kuchukua umbo jipya. Tatizo hili kwa sasa linaonekana katika mfumo wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; kazi za suluba kwa ujira mdogo, madeni makubwa kutokana na michezo ya upatu, watoto wadogo kufanyishwa kazi za nguvu na hata wakati mwingine, kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha mapigano na vita. Kuna wanawake, wasichana na vijana wanaofanyishwa kazi ngumu za majumbani kiasi cha kudhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Mifumo yote hii ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, hata kama hakuna takwimu rasmi kuhusu watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, lakini, Jumuiya ya Kimataifa ina uhakika kwamba, idadi ya watu hawa ni kubwa kuliko inavyodhaniwa. Waathirika wakuu ni wanawake, wasichana na watoto ambao wanakadiriwa kufikia milioni 40 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, tayari wamezamishwa kwenye ombwe la utumwa mamboleo. Hii ni changamoto inayowahusu watu wote wa Mungu na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kujitoa kwa kunawa mikono kwamba, hausiki. Kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali ukimya huu na kuanza kuishughulikia kashfa hii kwa ari na moyo mkuu, ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka na kudhalilishwa kutokana na utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya watu ambao wanahusika moja kwa moja, kwani wanafaidika sana na faida kubwa inayotokana na mifumo ya utumwa mamboleo. Hata wale ambao hawataki kusema, lakini wanajikuta wako katika mnyororo wa wale wanaofaidika kutokana na huduma inayotolewa na watu hao. Hii ni kashfa ambayo haiwezi kumwacha mtu salama anakiri Baba Mtakatifu Francisko. Hatua ya pili inapaswa kujielekeza zaidi kwa kuwasaidia waathirika wa mifumo ya utumwa mamboleo; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki zao msingi; kwa watuhumiwa wa biashara na mifumo ya utumwa mamboleo kufikishwa kwenye mkondo wa sheria, ili sheria iweze kufanya kazi yake. Wala rushwa na mafisadi washughulikiwe kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za kitaifa na kimataifa. Tatu, Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika mbali mbali ya kimataifa hayana budi kujikita katika kutafuta mambo yanayopelekea watu kutumbukizwa katika utumwa mamboleo ili kuyachemshia dawa yake!

Changamoto ya kwanza inayopaswa kuvaliwa njuga anasema Baba Mtakatifu ni umaskini wa hali na kipato unaosababisha hata kumong’onyoka kwa kanuni na tunu msingi za maisha ya maadili na utu wema. Vita, rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni mambo yanayopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, ili kufanya maboresho makubwa katika sera na mikakati ya uchumi, maendeleo endelevu kwa kujikita pia katika utawala wa sheria. Miundo mbinu iendelee kuimarishwa ili kuboresha maisha ya watu, vinginevyo, haitakuwa rahisi kupambana na watu ambao wamebobea katika biashara ya binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Waathirika wakuu ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu kwa moyo mkunjufu anasema, sera bora za maendeleo endelevu na elimu bora na makini vitasaidia kupambana na janga la utumwa mamboleo duniani, kwa kuongeza fursa za kazi na ajira, ili kuwajengea watu nguvu ya kiuchumi. Mchakato huu unahitaji: ujasiri, uvumilivu, udumifu na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kuwashirikisha wadau mbali mbali katika jamii. Kanisa linapaswa pia kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mapambano haya ili kuondoa ubaguzi na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu, ili kukuza na kudumisha: uhuru kamili, utu, heshima, haki, usawa na amani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jukwaa la Pili la Kimataifa Dhidi ya Utumwa Mamboleo linaloongozwa na kauli mbiu “Matatizo ya zamani katika ulimwengu mamboleo”, litaweza kupata mafanikio makubwa katika sera na mikakati yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.