2018-05-07 08:35:00

Parokia inayoinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa huduma kwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 6 Mei 2018 ametembelea na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika Parokia ya “SS. Sacramento” iliyoko Tor dè Schiavi, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma. Itakumbukwa kwamba, Parokia hii imewahi kutembelewa na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1972 kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Kunako mwaka 1974 Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa Parokiani hapo. Baba Mtakatifu alipowasili amepokelewa na Askofu mkuu Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Kardinali Josè Gregorio Rosa Chaves, Padre Maurizio Mirilli, Paroko pamoja na wasaidizi wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika ziara yake ya kichungaji Parokiani hapo, amezindua nyumba kwa ajili ya familia zenye ulemavu na watoto yatima, kielelezo cha parokia inayojitambulisha kama familia, chemchemi ya furaha na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Nyumba hii inaitwa “Casa della gioia” yaani “Nyumba ya furaha” ambayo imepata ufadhili pia kutoka kwenye Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, ndiyo maana Kardinali Luis Antonio Tagle amekuwepo ili kushuhudia tukio hili linalopania kumwilisha furaha ya Injili kwa watu wanaoteseka ndani ya jamii, ili wao pia waweze kuonja ushuhuda wa upendo unaotolewa na familia ya Mungu.

Huu ni msaada unaobubujika kutoka katika Injili kwa watu wenye imani na upendo walioguswa na mahangaiko ya jirani zao kiasi hata cha kuyavalia njuga anasema Padre Maurizio Mirilli. Hii ni nyumba inayotoa hifadhi kwa walemavu saba kutoka Parokiani hapo na inahudumiwa na Shirika la Watawa Wasalesiani wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, “Suore Salesiane dei Sacri Cuori” pamoja na mlei mmoja! Ndani ya jengo hili pia kuna kikanisa ambacho kitakuwa kinatumika kwa ajili ya Ibada ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu itakuwa ni chemchemi ya nguvu, furaha, ari na bidii katika kuwahudumia watu wanaohifadhiwa kwenye nyumba hii.

Wazazi wa watoto walemavu wanamshukuru Mungu kwa fursa hii, kwani wamepata makazi ambayo sasa yanawahakikishia usalama wa maisha ya watoto wao walemavu hata baada ya wazazi wao kufariki dunia, watakuwa na uhakika wa kupata huduma ya maisha ya kiroho pamoja na kuonja upendo kutoka kwa majirani. Hii ni parokia ambayo licha ya kuwa pembezoni mwa Jimbo kuu la Roma, lakini imesheheni shughuli mbali mbali za kichungaji zinazowafanya waamini kufurahia maisha parokiani hapo.

Kati ya vyama vya kitume vinavyovuma sana ni “Shule ya Sala” kwa Watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 5-7; Umoja wa Vijana Wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu; Kikundi cha Wataalam pamoja na Kikundi cha familia kinachopania kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia katika uhalisia wao, kama mbinu mkakati wa kupambana na utamaduni wa kifo unaozinyemelea familia nyingi kwa sasa. Si haba kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameandamana na ujumbe mzito kutoka Caritas Internationalis kwani, Parokia hii, iko mstari wa mbele katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni mahali ambapo, watu wenye shida na changamoto mbali mbali wanapata fursa ya kusikilizwa na kusaidiwa ili kupambana na changamoto za maisha yao ya kila siku kwa imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu wakati wa ziara yake ya kichungaji ameungamisha waamini waliokuwa wamejiandaa kupokea huruma na msamaha wa Mungu katika maisha yao; akatoa Sakramenti ya Kipaimara kwa mtoto mwenye ugonjwa hadimu, ili kumtia moyo na nguvu ya kusonga mbele katika imani kama askari wa Yesu. Amejibu maswali kutoka kwa waamini Parokiani hapo, akakutana na kuzungumza na wagonjwa pamoja na wazee.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.