2018-05-05 14:26:00

Maisha ya kitawa: utofauti na umoja wa karama kazi ya Roho Mtakatifu


Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuanzia tarehe 3-6 Mei 2018 linafanya kongamano la kimataifa kwa ajili ya maisha ya kitawa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Antonianum kilichoko mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe hawa Ijumaa, tarehe 4 Mei 2018 amekazia umuhimu wa maisha ya sala, ufukara na uvumilivu unaopaswa kuwa ni dira na mwelekeo wa kupambana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali katika maisha ya kitawa na kazi za kitume. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Consecratio et consecration per evangelica consiglia” yaani “Kuwekwa wakfu kwa ajili ya mashauri ya Kiinjili.”

Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika hotuba yake elekezi amekazia umuhimu wa watawa kushikamana na kushirikiana katika mchakato wa kutafuta mbinu mkakati wa kupyaisha maisha na utume wa kitawa, ili waweze kuonja kwa mara nyingine tena ile furaha ya Injili, tayari kuwashirikisha wale wote wanaokutana nao katika maisha na utume wao! Kwa mara ya kwanza, mkutano huu umevijumuisha vyama na mashirika ya kitume, ambayo yamekuwa ni chemchemi ya miito ndani ya Kanisa.

Karama mbali mbali zinazoendelea kuibuka ndani ya Kanisa ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Lakini, anasema Kardinali Joao Braz de Aviz kuna haja ya kuwa na sheria kanuni na miongozo inayopaswa kufuatwa ili kupambanua karama na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Leo hii, kuna watu wa ndoa ambao wamejiweka wakfu mbele ya Mungu na Kanisa kama mfumo wa maisha mapya ya kujiweka wakfu. Mfano halisi ni kile kinachojulikana kwa sasa kama “familia ya kikanisa”. Changamoto kubwa hapa ni jinsi ya kufahamu namna ya kumwilisha mfumo huu wa maisha kadiri ya sheria kanuni na miongozo ya Kanisa.

Waamini wanapaswa kukazia Sakramenti ya Ubatizo kuwa ni kiini cha wakfu wao mbele ya Mwenyezi Mungu unaowawezesha kuitwa wana wateule wa Mungu na ndugu zake Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Katika mtazamo na mwelekeo huu, waamini wanaweza kuwa na ufahamu mpana wa maisha yao ya wakfu katika utofauti na mkamilishano wake katika maisha ya watu wa Mungu.

Profesa Nuria Calduch Benages amedadavua kuhusu mwono mpana wa maisha ya wakfu unaojikita katika mwelekeo wa kinabii na ule wa kihekima kwa kukazia mambo msingi kama yanavyofafanuliwa kwenye Injili yaani: wakfu, wito na maisha ya kijumuiya utambulisho na chapa makini kwa ajili ya ufuasi na huduma kwa ajili ya watu wa Mungu. Kwa upande wake Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amekazia wakfu kama sehemu ya mchakato endelevu unaokumbatia na kuambata tofauti katika umoja unaonesha na kushuhudia amana na utajiri wa kitaalimungu, karama na mapaji yanayopaswa kuendelezwa na kudumishwa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Si rahisi sana kutoa maana ya karama zote hizi ndani ya Kanisa, lakini zinaweza kuelezewa na kufafanuliwa kwa dhati!

Kwa upande wake Sr. Carmen Ros Nortes, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amekazia umuhimu wa Kanisa kuendeleza mifumo mbali mbali ya maisha ya kitawa na kazi za kitume kama sehemu ya mchakato wa upyaisho unaobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu, daima Kanisa likiendelea kujitahidi kusoma alama za nyakati. Jambo la msingi ni kutambua mitindo na mifumo ya maisha ya kitawa inayokidhi mahitaji ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Wajumbe wa kongamano hili wamepata fursa pia ya kushiriki katika mkesha was ala uliofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwa kuongozwa na Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.