2018-05-05 15:23:00

Maisha na utume wa Masista wa Tutzing, Ndanda, Mtwara, Tanzania!


Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing lilianzishwa kunako mwaka 1884, huko St. Ottilien nchini Ujerumani. Shirika letu lilianzishwa na Padre Andreas Amrhein huko Ujuerumani, akiwa na lengo la kwenda kuinjilisha Neno la Mungu. Karama ya Shirika letu ni kuishi katika jumuiya chini ya kiongozi wa nyumba kama njia makini ya kujitakatifuza na kuendelea kuinjilisha, changamoto ambayo imepewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko kwa watawa kama mahali pa uinjilishaji, ushuhuda wa kinabii pamoja na kutakatifuzana tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Shirika letu limeenea karibu sehemu nyingi, mpaka sasa tupo nchi mbalimbali, miongoni mwa nchi hizo ni Kenya, Uganda, Brazil, Ufilippini, Angola, Korea, Namibia, Ujerumani, Marekani na Tanzania.

Katika nchi ya Tanzania tupo Jimbo Katoliki la Mtwara, wilaya ya Masasi, Ndanda na katika Jimbo kuu la Songea, tupo Peramiho. Katika mwaka 1901 Wamisionari walifika Peramiho na mwaka 1908 walifungua nyumba ya kwaza Ndanda. Sehemu ya kwanza wamisionari walitumwa Tanzania kwenda kumtangaza Kristo na kumsaidia mwanadamu: kiroho na kimwili kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaopania wokovu wa mtu mzima. Hivyo basi, utume wetu ni kufundisha, katika shule mbalimbali, kuhudumia wagonjwa na wenye shida mbalimbali na kazi za kichungaji, kama vile kufundisha katekesi na dini katika shule mbalimbali.

Changamoto kubwa iliyoko mbele yetu tunayopaswa kuibeba kwa uvumilivu, ari na moyo mkuu kama anavyosema Baba Mtakatifu ni upungufu wa miito miongoni mwa vijana wa kike wanaotaka kujisadaka na kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya Shirika la Masista wa Wamisionari wa Wabenediktini wa Tutzing, kwa kuishi mashauri ya Kiinjili. Hii ni changamoto tunayoifanyia kazi kwa kuwahamasisha vijana kusikiliza, kung’amua, ili hatimaye, kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kumfuasa Kristo Yesu kwa ukamilifu katika maisha ya kijumuiya kama njia ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha, mwito unaotolewa kwa namna ya pekee sana na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12). Hii ni changamoto inayopaswa pia kufanyiwa kazi katika maisha ya sala inayomwilishwa katika ushuhuda wa maisha na utume wetu!

Shirika letu linafanya Hija ya maisha ya kiroho kila mwaka hapa Roma, Masista toka nyumba mbalimbali tunakusanyika hapa Roma kwa lengo la kujifunza zaidi na kuzama katika mizizi ya shirika letu kama sehemu ya majiundo endelevu ya maisha na utume wetu. Tunatembelea sehemu za historia ya Mtakatifu Benedikto na pia kuimarisha imani yetu Katoliki hapa Roma kwa kutembelea maeneo ya kihistoria. Ni muda wa kusali na kutafakari zaidi maisha na utume wetu katika ulimwengu mamboleo, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kuwatumia jirani zetu ndani na nje ya Tanzania. Tunawakalibisha vijana wenye wito wa kumtumikia Mungu katika maisha ya kitawa kujiunga na Shirika letu la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing. Asanteni!

Mimi ni Sr. Bonifacia Ngonyani, OSB.

Ndanda, Mtwara, Tanzania. 








All the contents on this site are copyrighted ©.