2018-05-04 14:28:00

Abate mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, OSB aibuka kidedea!


Shirika la Wabenediktini wa Monasteri ya Hanga, Jimbo kuu la Songea, Tanzania limebahatika kupata jembe jipya katika taaluma baada ya Mheshimiwa sana Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, tarehe 3 Mei 2018 kutetea kazi yake ya shahada ya uzamivu kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma. Jopo la Maprofesa lililokuwa linaongozwa na Prof. Oborji Francis Anekwe limempongeza kwa kazi nzuri ambayo inajikita zaidi katika ushuhuda endelevu wa kimisionari unaotolewa na Monasteri ya Hanga, kama mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa utume na umisionari wa Kanisa unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa watu wake. Hii ni jumuiya inayojikita katika huduma makini kama kielelezo cha imani tendaji.

Ni Jumuiya inayotumwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kwa mtindo wake wa maisha, Jumuiya inakuwa ni mahali pa majadiliano, utamadunisho na huduma makini kwa watu wa Mungu. Sheria ya Mtakatifu Benedikto imekuwa ni nguzo na mhimili mkuu wa ushuhuda kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji Jimbo kuu la Songea. Utetezi wa kazi hii, umeshuhudiwa na “vigogo wa Shirika la Wabenediktini kutoka ndani nan je ya Roma, bila kuisahau familia ya Mungu kutoka Tanzania. Kwa hakika Mheshimiwa sana Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda amekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa wanafunzi wanaoendelea kujitaabisha katika masomo, ili siku moja waweze kuibuka kidedea kutetea kazi zao, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa ndani nan je ya Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.