2018-05-03 07:19:00

Vijana simameni kwa miguu yenu msikubali kuwa bendera kifuata upepo!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre  kutambua kwamba, wao ni vyombo vya huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa waja wake. Wajenge na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza kabla ya kutoa majibu ya haraka haraka, ili kusaidia mang'amuzi ya miito wakati wa maungamo, pale vijana wanapokimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu! Kanisa kama Mama na Mwalimu, anataka kuwasaidia vijana kusikiliza kwa makini, kile ambacho Mama Kanisa anataka kuwafundisha, kung'amua na hatimaye, kumwilisha ushauri huu, kama sehemu ya upya wa maisha yao, unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu!

Hivi karibuni Idara ya Toba ya Kitume, kwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika mchakato wa maisha ya vijana, imani na mang'amuzi ya miito, tema inayovaliwa njuga kwa sasa na Mama Kanisa katika maisha na utume kwa vijana, iliandaa kongamano la vijana ili kuwasaidia kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika safari ya maisha ya Kikristo na mang’amuzi ya miito mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume katika hotuba yake elekezi alitambua umuhimu wa vijana waamini katika maisha na utume wa Kanisa na kuwataka Mapadre ambao kimsingi ni mashuhuda, vyombo na manabii wa huruma ya Mungu kuwa na mwelekeo mpya katika kutekeleza dhamana na wajibu wao kama vyombo vya huruma, msamaha na upatanisho, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini! Kongamano hili limeongozwa na kauli mbiu “Kitubio kwa vijana, imani na mang’amuzi ya miito” kama sehemu ya maandalizi ya  maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi, mwezi Oktoba, 2018.

Kardinali Mauro Piacenza anasikitika kusema, vijana wanarithishwa ulimwengu ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu au kwa maneno mengine kama kichwa cha mwendawazimu! Kwa upande mwingine, kuna vijana ambao kwa asili ni watu ambao wako wazi na tayari kupokea na kukumbatia maisha wanayopaswa kuyaishi katika undani wake, lakini wanakabiliwa na vikwazo na vizingiti katika maisha. Vijana leo hii, wanaonekana kana kwamba, “si mali kitu” na wanachangia “kiduchu sana katika ustawi na maendeleo ya kijamii! Katika patashika hii nguo kuchanika anasema Kardinali Piacenza, Kanisa pia limetupiwa sana “madongo” na vijana kwa kutowajali, kuwasikiliza na kuwathamini katika hija ya maisha yao hapa duniani na kwamba, hawana tena thamani kama “ganda la ndizi”.

Kutokana na changamoto pamoja na uelewa huu, Mama Kanisa anatambua hatua mbali mbali za ukomavu wa imani miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo vijana, kiasi hata cha kuweza kujitambulisha na Imani ya Kanisa, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa jirani sanjari na kuzingatia mambo msingi katika maisha. Leo hii si rahisi sana kwa kijana kujitambua na kujitambulisha kuwa ni mwamini mkatoliki, anayetaka kumfuasa Kristo Yesu kwa dhati kabisa kutokana na kuogopa macho na maneno ya watu, kama ilivyokuwa kwa Mfalme Herode, hata baada ya kutambua kwamba, Kristo Yesu hakua na hatia iliyompasa kufa Msalabani, lakini ili aweze kuwafurahisha watu na kujijenga kisiasa akaamua Kristo Yesu, ateswe na kufa Msalabani.

Kardinali Mauro Piacenza anaendelea kusema kwamba, vijana wengi leo hii, wametopea katika ubinafsi na uchoyo; wanapenda kujitambulisha kwa makundi ya mitandao ya kijamii pasi na mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa kijamii. Na matokeo yake, ni vijana wengi kujikuta wakiogelea katika upweke hasi unaoweza hata kuwatumbukiza katika ugonjwa wa sonona. Ugonjwa humfanya mtu ashindwe kutimiza majukumu yake ya kila siku. Mfumo wa maisha ya watu umekuwa chanzo cha magojwa yanayowasumbua  watu wengi kiasi cha kukata tamaa katika maisha.

Vijana ambao wamekuwa kweli ni moto wa kuotea mbali kutokana na ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kujiunga na vyama mbali mbali vya utume kwa vijana, wamekuwa kweli ni msaada mkubwa kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hawa ni vijana wanaojifunza kwa kukosa na kukoseana; kwa kusahihishwa na kurekebishwa kidugu; kwa kuthaminiwa na kuheshimiwa hata katika udhaifu na mapungufu yao, daima wakipewa nafasi ya kuweza kukimbilia huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha. Vijana wa namna hii wanapata nafasi ya kutambua na kutumia karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ikilinganishwa na vijana wanaobweteka vijiweni kwa kupiga soga siku nzima!

Kardinali Mauro Piacenza, anawataka viongozi wa Kanisa kusoma alama za nyakati, kutambua na kung’amua mambo msingi katika maisha ya vijana, ili kuwasaidia kutekeleza kwa ufasaha zaidi ile ndoto kubwa ya maisha yao. Michezo ni jukwaa muhimu sana linaloweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kutambua karama na mapaji yao kwa ajili yao binafsi na jamii inayowazunguka. Viongozi wa Kanisa wajitahidi kuwekeza katika michezo kwa vijana inayoweza kusaidia pia kuratibu mahusiano yao na vijana wengine; kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema; kwa kuwajibika kikamilifu na kimaadili katika matumizi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwani hii inaweza kumjenga mtu, au kumbomoa mtu kimaadili na kiutu na hivyo kuonekana mtu wa ovyo kabisa!

Vijana wasaidiwe kujenga na kukuza dhamiri nyofu inayowajibika mbele ya Mungu na jirani zao, daima wakikazia mambo msingi katika maisha badala ya kukimbizana na mambo mpito, ambayo mara nyingi yanawaachia mahangaiko na majuto katika maisha! Vijana wajitahidi kusimama kwa miguu yao na wala wasikubali kuwa ni bendera kifuata upepo! Kutokana na changamoto mamboleo, utume kwa vijana ni dhamana inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana, ili kuweza kufikia matamanio yao halali katika maisha. Kumbe, kwa vijana ambao wako tayari kutambua udhaifu na mapungufu katika safari ya ujana wao na hivyo kukimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, huyu ni kijana ambaye amekomaa na ni mwana mapinduzi ambaye anafahamu kile anachopaswa kutenda na anakitenda kwa ari na moyo mkuu bila kuangalia maneno na macho ya watu! Hawa ni vijana wanaotambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu kwa waja wake. 

Vijana waliokuwa wanashiriki katika kongamano hili wamepata nafasi pia ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa watu mbali mbali ambao wamebahatika kukutana na Kristo Yesu, wakapata mwelekeo mpya wa maisha hawa ni kama Dr. Salvatore Martinez, Rais wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia. Wengine ni Chiara Amirante, Mwenyekiti wa Chama cha Kitume cha “Nuovi Orizzonti” kutoka Italia. Vijana wameshirikishwa kikamilifu kuhusu matatizo na changamoto wanazoweza kukutana nazo katika mchakato wa kumwilisha Sakramenti ya Upatanisho kama sehemu muhimu sana ya safari ya maisha yao hapa duniani. Vijana wamefafanuliwa changamoto, vikwazo na fursa wanazoweza kupata kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anataka kuwafundisha vijana maana ya maisha, ili waweze kutembea katika mwanga na kweli za Kiinjili tayari kutoa hata majibu magumu katika maisha yao kama ushuhuda wa imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.