2018-05-03 07:00:00

Salam na matashi mema ya viongozi wa Kanisa kwa huduma ya uamsho


Kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 1 Mei 2018, vikundi na jumuiya za Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS, zimekuwa zikikutana huko Pesaro, ili kusali, kutafakari na kumshukuru Mungu kwa huruma na upendo wake wa daima. Mwaka huu, wanaongozwa na sehemu ya Injili ya Luka juu ya mfano wa Msamaria mwema aliyemwonea huruma yule mtu aliyeangukia kati ya wanyang’anyi.  Hata leo hii, Yesu anawaambia wafuasi wake “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”. Changamoto ya huduma makini kwa Mungu na jirani ndiyo ambayo imefanyiwa kazi na wajumbe wa Chama Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia kwa wakati huu.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la walei, familia na maisha katika salam na matashi mema kwa wanachama wa Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia anasema, huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini na wale wanaoteseka kutokana na madhara ya dhambi ni ushuhuda wa Kristo Msamaria mwema, anayetaka kujenga na kudumisha uhusiano wa huruma na upendo na waja wake. Kristo katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha pekee kwa watu waliokuwa wanateseka: kiroho na kimwili; akawaponya magonjwa yao, akawapatia mahitaji yao msingi na hatimaye, akawasamehe dhambi zao.

Kardinali Kevin Joseph Farrell anakaza kusema, huruma ya Yesu ni chemchemi ya upendo unaowasukuma waamini kutoka katika ubinafsi wao, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha mahangaiko ya jirani zao: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anakazia umuhimu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha katika maisha yao “Heri za Mlimani” ambazo ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, hasa kwa kukazia umuhimu wa kusamehe wale waliowakosea kwa kutambua kwamba, hata wao, wanahitaji msamaha wa dhambi zao na huruma ya Mungu.

Kumbe, ni wajibu wa kila mwamini kujiunga na jeshi hili kubwa la watu waliosamehewa na kuonewa huruma na Mungu ili kweli waweze hata wao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Kwa hakika katika hija ya maisha yao katika jangwa la maisha na hali ya utupu, wameonja huruma kutoka kwa jirani zao, sasa huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, huruma hii inamwilishwa katika uhalisia wa maisha kama chachu ya utakatifu wa maisha ya Kikristo na kielelezo cha imani tendaji! Baba Mtakatifu anawataka waamini kupambana na ubinafsi, uchoyo na ubaridi katika maisha yao, ili kushuhudia zawadi ya imani inayomwilishwa katika jumuiya. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, kila mtu anashiriki kikamilifu katika ujenzi wa jumuiya yake na kamwe wasiwe ni sababu ya utengano na majeraha katika maisha ya kijumuiya!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Salvatore Rini Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya katika ujumbe wake, anakazia umuhimu wa Wakristo kuchuchumilia utambulisho wa Kristo Msamaria mwema kama sehemu ya utambulisho wao wa Kikristo na kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo, chachu ya utakatifu wa maisha. Waamini waguswe na mahangaiko ya jirani zao: kiroho na kimwili; wawe na ujasiri wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira kwani uchafuzi mkubwa wa mazingira ni chanzo kinachowatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato! Wakristo wawe ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Huduma ya upendo kwa maskini, ijenge na kuimarisha umoja, udugu na mshikamano, changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo!

Naye Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya anawapongeza wajumbe wa Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS, kwa tema “Yesu alipomwona na alimhurumia... akampeleka hata katika nyumba ya wageni, akamtunza... akamwambia Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”. Kwa hakika, huduma kwa Mungu na jirani ni ushuhuda wenye mvuto katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, anawataka wajumbe wa Chama hiki kujitahidi kumwilisha katika uhalisia wa maisha yao, sehemu hii ya Injili ya Msamaria Mwema, ambayo ni utambulisho wa Kristo Yesu mwenyewe; Neno wa Baba wa milele na Uso wa huruma ya Mungu aliyekuwa na huruma kwa binadamu katika masumbuko yake: kiroho na kimwili; akamwonea huruma, akamwalika katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani pamoja na kuwashirikisha majirani katika tiba, toba, uponyaji pamoja na kuwaweka huru, ili kuanza hija ya maisha mapya!

Kardinali Gualtiero Bassetti anakaza kusema, Kanisa nchini Italia, linatumaini sana ushuhuda wa imani yao inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha kama njia ya kuwasaidia watu kukutana na Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni kiini cha uinjilishaji mpya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo na kwamba, hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe wa Chama hiki cha kitume kuhakikisha kwamba, wanakita maisha yao katika: sala ya kijumuiya, matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kuenea katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Huduma kwa Mungu na jirani ni ushuhuda wenye mvuto unaopaswa kuendelezwa zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.