2018-05-02 11:03:00

Rais Mafuguli atema cheche! Miradi ya maendeleo kupewa kipaumbele!


Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuzalisha ajira 1,826,743 katika kipindi kifupi cha miaka miwili na nusu iliyopita. Rais Magufuli amefafanua kuwa kati ya ajira zilizozalishwa, wafanyakazi 18,101 ni watumishi wa umma wapya walioajiriwa kupitia kada mbalimbali, sekta binafsi imetoa ajira mpya 582,073 na ajira nyingine zimezalishwa kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja, umeme, ujenzi wa shule na vyuo, afya, viwanja vya ndege, viwanda, kilimo, mifugo na madini. Rais Magufuli ameyasema haya Mei Mosi, 2018 mjini Iringa wakati wa sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi ambayo kwa mwaka huu, imeadhimishwa mjini Iringa.

Aidha Rais Magufuli amesema katika kipindi hicho Serikali imewapandisha vyeo wafanyakazi 88,016 na wengine 25,504 watakaopandishwa ifikapo Julai 2018 na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwapandisha vyeo wafanyakazi kadri bajeti itakavyoruhusu. Kuhusu malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania imeshawalipa wafanyakazi 52,851 waliokuwa wakidai Shilingi Bilioni 220.627 za madeni ya mishahara na yasiyo ya mishahara yaliyolimbikizwa tangu mwaka 2007 na amewahakikishia watumishi wote wanaodai madeni halali kuwa watalipwa fedha zao.

Rais Magufuli amesema, Serikali imeamua kuelekeza fedha nyingi katika kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo na amewataka wafanyakazi kuongeza juhudi na maarifa kazini ili kuongeza tija, ufanisi na uzalishaji mali, na pia ameahidi kuwaongeza mshahara kabla kumaliza kipindi chake cha uongozi. Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu Kassim M. Majaliwa kuchukua hatua dhidi ya viongozi wanaowahamisha wafanyakazi pasipo kuwalipa stahili zao na ameonya kuwa hatarajii kusisikia mtumishi mwingine amehamishwa bila kulipwa stahili zake.

Rais John Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama kuhakikisha mifuko ya hifadhi ya jamii iliyounganishwa kutoka 5 na kubaki 2 ambayo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Sekta Binafsi (NSSF), inaanza kufanya kazi haraka.
Kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa, Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya mkoa huo ikiwemo kuimarisha miundombinu ya utalii, kujenga barabara na kusambaza umeme katika vijiji 179 vilivyobaki.

Katika taarifa yao iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Dr. Yahya Msigwa, wafanyakazi nchini Tanzania wamempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake zikiwemo kubana matumizi yasiyo ya lazima, kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii, kupigania rasimali za Taifa, kuondoa watumishi hewa, vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya na ujenzi wa miundombinu, na wamemuahidi kumuunga mkono na hawatawatetea wafanyakazi wazembe, wavivu, watovu wa nidhamu, jeuri na wala rushwa.

Na mwandishi maalum, Iringa, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.