2018-04-30 13:22:00

Papa Francisko kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi, Ostia, 3 Juni 2018


Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila Mwaka Mama Kanisa anayofuraha kubwa ya kusherehekea na kushuhudia Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa maandamano makubwa, ushuhuda kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuandamana na waja wake katika historia ya maisha yao ya kila siku hadi utimilifu wa dahali.

Ekaristi Takatifu ni kiini cha imani ya Kanisa Waamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili tarehe 3 Juni 2018 wataadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Sherehe hii kwenye Parokia ya Mtakatifu Monica, huko Ostia, nje kidogo ya mji wa Roma. Baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu ataongoza maandamano ya Ekaristi Takatifu na kuhitimishwa kwenye Parokia ya “Nostra Signora di Bonaria” na baadaye atatoa baraka ya Ekaristi Takatifu.

Kila Jumapili, waamini wanaadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, Siku ile ya Alhamisi kuu wakati wa Karamu ya Mwisho! Lakini, kila mwaka, Kanisa lina furaha kubwa ya kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, kiini cha imani ya Kanisa kwa kumwabudu Kristo Yesu anayejisadaka na kujitoa kwa waja wake kama chakula na kinywaji cha wokovu! Kristo Yesu ni mkate na kinywaji kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele; ni sadaka ya Kristo mwenyewe kwa ajili ya binadamu! Mwana wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu ni Mwana Kondoo wa Pasaka, anayemkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa lindi la dhambi na mauti na kumwongoza katika Nchi ya ahadi.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili  kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ni uwepo endelevu wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya waamini mahali popote pale walipo: mjini na vijijini; Kaskazini na Kusini mwa dunia; katika nchi ambazo kimsingi zina utamaduni na Mapokeo ya Kikristo na hata katika Nchi zile ambazo zimeinjilishwa hivi karibuni. Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Yesu anajisadaka mwenyewe kama nguvu ya maisha ya kiroho ili kuwajengea uwezo wafuasi wake wa kumwilisha Amri ya upendo: kwa kupenda kama alivyopenda Yeye mwenyewe; kwa kujenga na kudumisha jumuiya inayomsimikwa katika ukarimu, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kulishwa na Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kujiaminisha kwake na kumwachia nafasi ili aweze kuwaongoza. Huu ni mwaliko wa kumpokea na kumpatia Kristo Yesu nafasi ya kwanza katika maisha, tayari kupokea na kumwilisha upendo unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, dhamana ya Roho Mtakatifu anayerutubisha na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani; watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao! Kwa kulishwa na kunyweshwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, waamini wanakuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kuhamasishwa kujenga na kudumisha umoja na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kama ambavyo waamini wanavyokumbushwa na Mtakatifu Paulo, Mtume! Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo na umoja. Hii ni kumbu kumbu yenye uvumilivu kwani hata katika magumu ya maisha, bado waamini wanatambua kwamba, Roho wa Kristo yuko ndani mwao.

Ekaristi Takatifu inawatia shime kusonga mbele kwani hata katika safari ambayo ni ngumu kiasi gani, waamini wanatambua kwamba, hawako pweke, na kamwe Kristo Yesu hawezi kuwageuzia kisogo na kwamba, kila wakati wanapomwendea anawapatia nguvu mpya kwa njia ya upendo wake. Ekaristi Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, hawapo peke peke, bali ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; familia ya Mungu kama ilivyojionesha kwenye Agano la Kale ilipokusanyika kwa ajili kuokota manna iliyoshuka kutoka mbinguni.

Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, anawaalika waamini kumpokea kwa pamoja na kumshikiri kati yao. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbu kumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.