2018-04-24 14:05:00

Mh. Padre Prosper Bonaventure Ky ateuliwa kuwa Askofu wa Dèdougou


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa sana Padre Prosper Bonaventure Ky kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Dédougou lililoko nchini Burkina Faso. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Prosper Bonaventure Ky kutoka Jimboni humo, alikuwa ni Katibu mkuu mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo nchini Burkina Faso na mkurugenzi wa nyumba ya Mapadre wanafunzi, Jimbo kuu la Ouagadougou. Askofu mteule Prosper Bonaventure Ky alizaliwa tarehe 10 Januari 1965 huko Toma, Jimbo Katoliki la Dédougou.

Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 23 Julai 1994. Tangu wakati huo, katika maisha na utume wake kama Padre amebahatika kuwa ni Jaalimu wa Seminari Ndogo ya Nasso, huko Bobo Dioulasso; Paroko usu, Jalimu na Gombera wa Seminari Ndogo ya Tionkuy, Jimbo Katoliki la Dédougou. Kati ya mwaka 2003 hadi mwaka 2010 alitumwa na Jimbo lake kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Wasalesiani na kuhitimu shahada ya uzamivu katika masomo ya Saikolojia. Kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2012 amekuwa ni Paroko usu wa Parokia ya Toma. Kuanzia mwaka 2012 hadi kuteuliwa alikuwa ni mkurugenzi wa nyumba ya Mapadre wanafunzi, Jimbo kuu la Ouagadougou.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.