2018-04-23 10:55:00

Kilio cha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya wanawake!


Dhamana, wajibu, changamoto na matatizo wanayokabiliana nayo wanawake Amerika ya Kusini ndicho kilichokuwa kiini cha mkutano wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini kilichofanyika hapa mjiniVatican kuanzia tarehe 6-9 Machi 2018 kwa kuwashirikisha wanawake ili kujadili mustakabali wao kwa sasa na kwa siku za usoni. Mkutano huu uliongozwa na kauli mbiu “Mwanamke, mhimili wa ujenzi wa Kanisa na Jamii Amerika ya Kusini”. Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini huko Bogotà wakati wa hija yake ya kitume! 

Papa aliwakumbusha kwamba, matumaini ya Amerika ya Kusini yanafumbatwa katika sura ya mwanamke. Mkutano huu umefanyika katika mazingira ya uhuru kamili kwa kuwapatia wanawake kuelezea: matatizo, changamoto na fursa zilizoko mbele yao katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Injili ya Kristo iwe ni mwongozo rejea katika majadiliano ya kuwajengea uwezo wanawake kwani Kristo Yesu aliwajali na kuwathamini sana wanawake, akawapatia uhuru wa kushiriki katika maisha na utume wake, kiasi ya kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko, kiini cha imani na maisha ya Kanisa. Alijali na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu.

Baada ya mkutano huu, wajumbe pamoja na mambo mengine, wamependekeza kufanyike Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Wanawake. Lengo ni kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wanawake. Kanisa liwe na ujasiri wa kupambana na nyanyaso, dhuluma na uonevu wanaokumbana nao wanawake katika maisha na utume wao! Umefika wakati kwa Mama Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wanawake wanaoteseka kutokana na mifumo mbali mbali ya ukandamizaji: katika familia, maeneo ya kazi na hata katika maisha ya hadhara. Umaskini wa wanawake wa Amerika ya Kusini ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuwakoa kutoka katika utumwa mamboleo.

Wajumbe, wameshauri kama sehemu ya mikakati ya shughuli za kichungaji kukazia majiundo awali na endelevu katika Sakramenti ya Ndoa kwa kukazia: uzuri, utakatifu, ukweli na changamoto za Injili ya familia ndani na nje ya Kanisa. Lengo ni kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili wazazi waweze kuwajibika barabara katika malezi na makuzi ya watoto wao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia zao. Changamoto kati ya kazi na wajibu wa kifamilia zinapaswa kuangaliwa vyema, ili kupambana na ubinafsi, uchoyo na utamaduni wa kifo unaotishia umoja na mafungamano ya wana ndoa! Kanisa litambue dhamana na wajibu wake kuwa ni “Mama na Mwalimu” kama ilivyo hata kwa Bikira Maria.

Wajumbe, wamewahimiza wanawake Amerika ya Kusini kuendelea kujikita katika malezi na makuzi ya watoto wao; kwa kukazia pia mahusiano mema kati ya wakleri, watawa na wanawake katika jamii, ili kusaidiana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Jumuiya za Kikristo hazina budi kuwa makini na dhana ya usawa wa kijinsia unaotaka kung’oa tofauti msingi kati ya mwanaume na mwanamke kwa kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo, kwani hizi ni dalili za ukoloni mamboleo unaoenea kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia. Ndoa za watu wa jinsia moja si sehemu ya haki msingi za binadamu! Sera za utoaji mimba na kifo laini ni kinyume kabisa cha Injili ya uhai na haki msingi za binadamu! Wajumbe wamekazia sheria kanuni na msingi wa maadili na utu wema. Kumbe, Kanisa lisichoke kufanya majadiliano ya kina na endelevu na wanasiasa wanaotaka kukumbatia utamaduni wa kifo. Wanawake washirikishe pia katika malezi na majiundo ya wakleri kama inavyokaziwa kwenye “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre”.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu“Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis”: “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre”  yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”,  anasema, malezi na majiundo ya kipadre kwanza kabisa ni kazi ya Mwenyezi Mungu ambayo inamtaka jandokasisi au Padre kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumfunda kadiri anavyotaka! Pili, Kasisi mwenyewe anapaswa kutambua kwamba, ni mhusika mkuu wa majiundo katika wito, maisha na utume wake wa kipadre. Tatu, wadau wakuu wa malezi ni walezi waliopewa dhamana hii kwa kusaidiana na Maaskofu huku wakitambua kwamba, wito unazaliwa, unakua na kukomaa ndani ya Kanisa ambaye ni mama na mlezi wa miito yote mitakatifu!

Wajumbe wanasema, kuna haja ya kumwilisha changamoto ya “dhana ya Sinodi” kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuiwezesha familia ya Mungu kushiriki kikamilifu katika kupanga, kujadili na kutekeleza sera na mikakati ya maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Malezi na makuzi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo, kitaaluma, kitaalimungu na kijamii, ni muhimu sana ili kuwawezesha wanawake na watawa kupambana na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo kwa kuwa na nyenzo msingi. Wanawake wawe mstari wa mbele kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kwa kujikita katika mchakato wa utamadunisho, kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na maisha kwa watu wa nyakati hizi! Kuna haja kwa Makanisa mahalia kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuwawezesha wanawake na viongozi wa Kanisa kushirikiana na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa mahalia na jamii katika ujumla wake. Wanawake wasipothaminiwa na mchango wao kutambuliwa na Kanisa, wataligeuzia kisogo Kanisa, na kutokomea “kusikojulikana”.

Mwishoni, wajumbe, wameliomba Kanisa kusaidia kumwilisha ari na mwamko wa kimisionari kama unavyodadavuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” unaohimiza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; katika furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni wakati wa kuimarisha Injili ya familia kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika  Waraka wake wa kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” kwa kutambua kwamba, familia bado ni kiini cha Habari Njema hata katika ulimwengu mamboleo.

Ni mwaliko kwa familia ya Mungu kuthamini na kudumisha zawadi ya ndoa na familia kwa kujikita katika utakatifu, uzuri na udumifu wake unaoimarishwa kwa fdhila za ukarimu, uwajibikaji, uaminifu na busara; kwa kusaidiana na kusindikiza katika mchakato mzima wa utakatifu wa maisha unaotambua karama, fadhila na mapungufu yanayojikita katika maisha ya mwana ndoa! Kumbe, Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya wanawake ni hitaji muhimu kwa wakati huu ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zilizopo miongoni mwa wanawake, ili kuweza kutekeleaza vyema dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake! Hati hii yenye mapendekezo ya mkutano wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini ni ushuhuda wa mchakato wa utamaduni wa watu kukutana, kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!









All the contents on this site are copyrighted ©.