2018-04-21 09:31:00

Papa Francisko: Vijana Cuba ipendeni nchi yenu na Kanisa la Kristo!


Askofu Alvaro Julio Beyra Luarca, Mwenyekiti wa Tume ya vijana Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba, tarehe 20 Aprili 2018 amepokea ujumbe kwa njia ya video kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko akiwatia shime vijana kumpenda Kristo Yesu na kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kanisa la Kristo nchini Cuba. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuondoa woga wa kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu anayewataka kujitosa katika huduma makini kwa Mungu na jirani zao katika hali na mazingira mbali mbali ambayo Mwenyezi Mungu anajifunua kwao!

Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanayoongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38 sanjari na maadhimisho yatakayofanyika huko Santiago, Cuba iwe ni fursa ya kuimarisha mchakato wa imani ya vijana na hatimaye, kwenda mbali zaidi ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa nchini Cuba, kwa leo na kesho.

Vijana wawe na moyo wa uzalendo na upendo kwa nchi yao kwa kutambua kwamba, wako watu wengi wanaoshiriki katika ujenzi wa nchi yao, kwa kuanzia katika jumuiya wanamoishi na kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kila siku na kwamba, huko ndiko mahali ambapo hata miito inachipua, inakua na kupaliliwa. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu; wakiipenda nchi yao na Kristo Yesu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu anawaweka vijana wa Cuba chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aendelee kuwatia shime!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.