2018-04-20 08:44:00

Siku ya Kuombea Miito Duniani: Mashemasi 16 kupewa Daraja Takatifu


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, tarehe 22 Aprili 2018 anasema, Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, daima amekuwa akiwasindikiza waja wake hata katika njia ngumu za maisha yao, zinazosheheni mavumbi na matope. Anatambua fika kiu ya upendo iliyoko ndani mwao na hivyo, anawaita kushiriki furaha yake isiyokuwa na kifani.  Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina mambo makuu matatu: kwanza kabisa: kujenga utamaduni na sanaa ya kusikiliza; pili, kufanya mang’amuzi ya miito na tatu ni kuishi upya wa maisha kama unavyopata utimilifu wake katika ufunuo wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, ujumbe huu ni mwendelezo wa tafakari kwa ajili ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii itakuwa ni nafasi ya kutafakari kwa kina mwaliko wa furaha kama kiini cha maisha kwa watu wa marika mbali mbali. Maisha na uwepo wa watu hapa duniani ni kadiri ya mpango wa Mungu na wala si kwa nasibu tu! Mwenyezi Mungu daima anapenda kukutana, kutembea na kuambatana na waja wake ili kuzima kiu ya upendo inayowaka ndani mwao.

Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu mchungaji mwema, majira ya saa 3:30 kwa saa za Ulaya, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kutoa Daraja takatifu ya Upadre kwa Mashemasi wa mpito 16 na kati yao 11 ni kwa ajili ya Jimbo kuu la Roma. Tukio hili linatanguliwa na mkesha wa sala Ijumaa, tarehe 20 Aprili 2018 kwenye Kikanisa cha Seminari kuu ya Jimbo kuu la Roma, ili kuombea miito mbali mbali ndani ya Kanisa na linaongozwa na Askofu mkuu Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.