2018-04-17 16:30:00

Nabii daima anasema ukweli na kulia kwa ajili ya watu wake wanapokosea


Nabii wa kweli ana uwezo wa kulilia watu wake wasio msikiliza. Huu ni uthibitisho wa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican tarehe 17 Aprili 2018 akitafakari sura  ya mfiadini wa kwanza mtakatifu Stefano na kwamba Kanisa linahitaji wote kuwa manabii ili kuweza kuongeza nguvu katika  ushiriki wa Mungu.

Mtakatifu Stefano alikuwa akiwalaumu watu  hao, yaani wazee na waandishi walio mpeleka katika mahakama kwamba: mliotahiriwa  katika mioyo na masikio lakini mnakuwa wagumu zaidi kupokea Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anaongeza kusema: hawa walikuwa wamefunga mioyo yao na hawakutaka kusikiliza, pia hawakuwa  na kumbu kumbu ya historia ya waisraeli.

Kama ilivyo tokea kwa manabii kuteswa kwasababu ya ukweli kwa njia ya babu zao, ndiyo hata wazee na manabii wakatili ndani ya mioyo yao wote walimshambulia Stefano na kumvuta nje ya mji na kumpiga mawe. Baba Mtakatifu anaongeza kusema, manabii wakisema ukweli na kugusa mioyo au kufunguka au moyo kugeuka wa mawe, ndipo inatokea hasira ya kumsababishia kifo cha nabii.

Kwa kawaida nabii wa kweli analia na watu wake kwasababu, ukweli uleta usumbufu kwa wengi wasio taka kusikiliza na ndiyo maana manabii daima wamepata matatizo na kuteswa kwasababu ya kusema ukweli. Kwa mujibu wa Baba Mtakatifu anathibitisha kwamba, nabii wa kweli na mwenye nguvu ni wale wenye kuwa na uwezo wa kusema ukweli  pia kulilia watu wake, ambao wanaacha ukweli. Yesu kwa upande mwingine anawakaripia kwa kutumia maneno magumu akisema: kizazi kilichopotea na kiovu, lakini kwa upande mwingine analilia Yerusalemu. Maandishi haya ni ya moja kwa moja ambayo yanathibitisha ukweli.

Hata hivyo pia  nabii wa kweli si yule wa maajabu, walakini ni mtu wa matumaini na kufungua milango, anaponya majeraha ya mizizi, anaponyesha mahusiano ya watu wa mungu ili waweze kwenda mbele. Nabii hana kazi ya kukaripia tu , lakini pia ni mtu wa kuonesha matumaini ya wakati uliopo na ujao. Ndiyo yeye anakaripia inapobidi, lakini pia anafungua mlango wa kutazama upeo wa matumaini. Kwa maana hiyo nabii wa kweli anafanya kazi yake vizuri inapogusa ngozi yake.

Kanisa la Mungu linahitaji huduma ya kinabii, kwa maana Mtakatifu Stefano alikufa mbele ya macho ya Sauli, kutokana na kutetea ukweli. Kutokana na ukweli huo,  Baba Mtakatifu Francisko ametaja sentensi mojawapo kati ya mababa wa Kanisa aliyesema kuwa: damu ya wafia dini ni mbegu ya wakristo.

Kanisa linahitaji manabii,na katika mfano hai, Kanisa linahitaji watu wote kuwa manabii. Si katika kulaumu kwa sababu ni jambo jingine maana  daima wapo ambao ni hakimu wa kulaumu mara nyingi hawapendi chochote, au kukubali chochote, badala yake ni kutaka kuagiza.... 

Nabii ni yule anayesali, anamtazama Mungu, anawatazama watu wake, anahisi uchungu wa watu wake wanapokosea, analia nao na pia  uwezo wa kulilia watu wake na zaidi mwenye uwezo wa kusema ukweli bila kuogopa. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amehitimisha akiomba neema ili huduma ya manabii wa Kanisa isikose kamwe  ili kuendeleza mbele katika huduma hiyo.

Sr Angela Rwezaula 
Vatican news!








All the contents on this site are copyrighted ©.