2018-04-16 11:28:00

Maaskofu Burundi: Ukweli na uwazi katika fedha ya uchaguzi mkuu


Mama Kanisa anathamini sana mfumo wa kidemokrasia kwa sababu unawahakikishia wananchi ushiriki wao katika maamuzi ya kisiasa, huwahakikishia watawaliwa uwezekano wa kuwachagua na kuwawajibisha wawatakao, na kuwabadilisha kwa njia ya amani wakati ukiwadaia. Kanisa haliwezi kupendelea uwepo wa vikundi vidogo vya watawala vinavyoweza kuendeleza itikadi zao. Kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, demokrasia halisi inawezekana tu katika serikali inayotawala kwa mujibu wa sheria, na kwa misingi ya dhana sahihi ya mtu nafsi. Ni sharti pawepo na mazingira ya lazima kwa maendeleo ya mtu binafsi kwa njia ya elimu na malezi katika maadili ya kweli, na ya sehemu ya ubinadamu katika jamii kupitia miundo ya uumbaji ya ushiriki na ushirikishanaji wa majukumu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi, linasema, familia ya Mungu nchini humo, kunako mwaka 2020 itafanya uchaguzi mkuu, fursa ya wananchi kutekeleza wajibu na dhamana yao ya kiraia kwa mujibu wa Katiba ya nchi, ambayo kimsingi ni sheria mama! Askofu Joachim Ntahondereye, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi anasikitika kusema kwamba, ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kugharimia mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Burundi umeingia kasoro kubwa kwa baadhi ya wananchi kuchangishwa maradufu. Kuna baadhi ya wananchi ambao wanalipishwa kodi kwa nguvu zaidi ya mara moja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria kanuni za nchi.

Uchaguzi mkuu ni tukio muhimu sana katika utekelezaji wa demokrasia, kumbe, ni zoezi ambalo linapaswa kupangwa vyema ili kuhakikisha kwamba, hata utekelezaji wake pia unakuwa makini na kwa wakati. Serikali inapaswa kuibua mbinu mkakati endelevu utakaowawezesha wananchi kuchangia vyema gharama ya demokrasia na kwa wakati huu maandalizi ya uchaguzi mkuu. Ili kufanikisha zoezi hili, vigezo vya ukweli na uwazi, vinapaswa kuzingatiwa! Serikali ioneshe kiasi cha fedha kinachotakiwa kukusanywa na kuweka mchanganuo na malengo yake, ili wananchi waweze kushiriki kwa moyo mmoja badala ya mtindo wa sasa ambao umeibua manung’uniko kutoka kwa wananchi wa Burundi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linasema, Kanisa kama sehemu ya dhamana, maisha na utume wake kwa familia ya Mungu nchini Burundi, litaendelea kujikita katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Mchango wa Kanisa katika mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Burundi unapaswa kuzihusisha Parokia ambazo zinaunda majimbo na hatimaye, Kanisa la Mungu nchini Burundi. Si haki kwa serikali kuomba mchango kutoka katika Parokia, Jimbo na Kanisa la Burundi katika ujumla wake. Si vyema na wala jambo la busara kwa Serikali ya Burundi kutoza kodi nyumba za watoto yatima, taasisi za elimu na afya! Hii ninatoka na ukweli kwamba, taasisi zote hizi zinachangiwa na Parokia kwa moyo wa ukarimu na upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.