2018-04-13 15:38:00

Mwenyeheri Lucien Botovasoa, Baba wa familia, shuhuda amini wa Kristo


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anasema, neema ya utakaso inaweza kuwasaidia waamini kuambata njia ya utakatifu, kwa kukumbatia Matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Wakristo watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani, kumbe, wanatumwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kadiri ya historia na changamoto za Kiinjili; daima kwa kuungana na Kristo Yesu katika Fumbo la maisha na utume wake, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma ya Baba kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu!

Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kuishi upendo katika utimilifu wake kadiri ya nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu. Maisha ya kila mwamini yawe ni kielelezo cha utume kutoka kwa Kristo Yesu anayetaka kuwaletea waja wake mabadiliko katika maisha, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kuambata upendo wa Kristo katika maisha yao! Ni katika mwelekeo huu, Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumapili, tarehe 15 Aprili 2018 hukoVohipeno, nchini Madagascar anamtangaza Mtumishi wa Mungu Lucien Botovasoa, shahidi, mwamini mlei, baba wa familia na mwanachama wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyeheri.

Mwenyeheri mtarajiwa Lucien Botovasoa alizaliwa kunako mwaka 1908 huko Vohipeno, nchini Madagascar, akabatizwa tarehe 15 Aprili 1922 na kubahatika kupokea Komunyo ya kwanza siku hiyo hiyo! Akaimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kunako mwaka 1923 na kukabiliana uso kwa uso na kifodini hapo tarehe 16 Aprili 1947. Mwenyeheri Luciano Botovasoa anaendelea kutajirisha orodha ya wenyeheri kutoka nchini Madagascar, kwani wapo pia: wenyeheri Victoria Rasoamanarivo pamoja na Rafael Rafiringa.

Kardinali Angelo Amato, anasema, Mwenyeheri Lucien Botovasoa ni mwanafunzi aliyefundwa na kufaulu vyema kutoka katika shule ya Kristo Yesu, Bwana na mwalimu, akajifunza kuwafundisha watu tunu msingi za maisha ya kiutu na kiinjili; akawataka watu wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani; kwa kujenga na kudumisha Jumuiya inayosimikwa katika upendo, udugu, umoja na mshikamano; ukarimu pamoja na kuheshimiana.

Alikuwa ni chachu ya maridhiano kati ya watu kwa kutokukumbatia ndani mwake chuki na uhasama; akajitahidi kuwaonjesha watu wote upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, umoja na mshikamano unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba; daima akijitahidi kusimama kidete kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Alikuwa ni mwalimu na shuhuda wa maisha katika ukweli na uwazi; Baba mwema wa familia aliyejali na kuihudumia familia yake kwa imani, upendo na matumaini makubwa!

Mwenyeheri Lucien Botovasoa alibahatika kuwa na kipaji cha akili, akafundwa kwenye Chuo cha Wayesuit huko Fianarantsoa na akafanya yote “Ad Majorem Dei Gloriam” yaani  kwa ajili ya “Sifa na utukufu wa Mungu”. Akiwa na umri wa miaka 22 akafunga ndoa na Bi Suzanne Soazana na kubahatika kupata watoto nane. Katika maisha ya ndoa, akajitahidi kutakatifuzana na mwenza wake kwa kukumbatia tunu msingi za Injili ya familia na leo hii ni mfano bora wa kuigwa kama chombo na shuhuda wa Injili ya familia. Alikuwa anafunga na kusali ili kuratibu vilema vya maisha yake, akajitahidi kuishi nadhiri ya ufukara; daima akawa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa wale waliokata tamaa.

Kardinali Angelo Amato anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyeheri Lucien Botovasoa aliuwawa wakati wa mapinduzi ya uhuru wa Madagascar hapo tarehe 30 Machi 1947, Jumapili ya Matawi! Akakamatwa na kushughulikiwa kama “chuma chakavu” kutokana na imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Akauwawa kikatili, huku akiendelea kusali, akimwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwasamehe watesi wake, na kwamba, damu yake inayomwagika ardhini, iwe ni mbegu ya wokovu kwa ndugu zake. Akauwawa kwa kutundikwa miguu juu na kichwa chini na baadaye, mwili wake ukatupwa mtoni!

Mwenyeheri Lucien Botovasoa, kijana mbichi kabisa, Baba wa familia, mwingi wa utajiri wa utu na utakatifu ni mfano bora wa kuigwa katika ulimwengu mamboleo kwa kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Ni chombo cha upendo na mshikamano wa kweli dhidi ya ubaguzi; akauwawa kikatili kwa vile tu, alikuwa ni shuhuda wa ukweli na haki; akawa mfano bora wa kuigwa katika msamaha na upatanisho, chachu muhimu sana ya ujenzi wa haki, amani, udugu na mshikamano kwa wote! Huu ndio muhtasari wa sheria kanuni ya Injili iliyomwilishwa katika maisha ya Mwenyeheri Lucien Botovasoa kutoka Madagascar.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.