2018-04-13 15:23:00

Maandalizi ya Sinodi ya Amazonia yaanza kushika kasi!


Maadhimisho ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia, yalianza rasmi wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù, alipotembelea na hatimaye kukutana na wananchi mahalia kule Puerto Maldonado. Kanisa linapenda kuendelea kujenga na kudumisha utamaduni na dhana ya Sinodi, kama njia ya watoto wa Kanisa kukutana, kujadiliana, kuamua na kutekeleza maamuzi yao kwa pamoja, kila mtu kadiri ya dhamana, wito na nafasi yake katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii ndiyo dhana inayofumbatwa katika utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyohitimishwa hivi karibuni, kwa vijana zaidi ya 350 kutoka sehemu mbali mbali za dunia kukutana, kujadiliana na hatimaye, wakatoa hati ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, hapa mjini Roma! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 12 Aprili 2018 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia.

Kati yao Baba Mtakatifu anasema, kuna wajumbe 18 kutoka Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu na wataalam 13. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anakaza kusema, Amazonia ni bustani kubwa inayofumbata utajiri mwingi unaobubujika kutoka katika mali asili, mila, desturi na tamaduni njema za wananchi asilia; watu wenye historia na nyuso za kupendeza! Lakini, hili pia ni eneo ambao linakabiliwa na hatari kubwa ya kuweza hata kutoweka kutokana na uchu wa kutaka kuchuma rasilimali zilizoko kwa ajili ya faida ya watu wachache pamoja na ukoloni mamboleo, unaotaka kutawala maisha ya wananchi wa Amazonia!

Katika utangulizi huu, Padre Justino Rezende, kutoka katika kabila la Tuica, anayewawakilisha wananchi mahalia, amewashukuru wajumbe wote wanaohudhuria mkutano wa maandalizi kwa kusema kwamba, hata yeye ni sehemu ya wajumbe hawa na kwa namna ya pekee, anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyeamua kutisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia, ili familia ya Mungu katika ujumla wake, iweze kudadavua: matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika Ukanda wa Amazonia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili.  Sinodi hii ni alama muhimu sana ya dhana ya Kanisa la Kiulimwengu linalotemba kwa pamoja katika maadhimisho ya Sinodi. Wananchi mahalia, wameinjilishwa, lakini sasa nao wanataka kujikita katika mchakato wa uinjilishaji kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, huku wakichangia amana na tunu msingi za maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 iongozwe na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia endelevu”.  Maandalizi ya nyaraka mbali mbali yatapata chimbuko lake katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia na kwamba, waamini walei ndio wanaoguswa na kuathirika zaidi kutokana na changamoto za kimissionari, kijamii na kiutu huko Amazonia, kumbe, wanategemewa sana na Mama Kanisa kwamba, watashirikisha uzoefu na mang’amuzi yao kutoka katika medani mbali mbali za maisha, ili kuweza kufanikisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia.

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita katika masuala ya haki, amani na mshikamano; utume na huduma ya upendo, ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inatamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia, ili Kanisa liweze kupata sura mpya ya watu wa Amazonia kwa kuwa na: wakleri pamoja na watawa wake! Hii ni changamoto inayohitaji ari, ujasiri na moyo wa kuthubutu, kwani kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na ukoloni mamboleo, unaofumbatwa katika nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayotishia: ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Amazonia. Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia inapania pamoja na mambo mengine; kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na kitume kwenye Ukanda wa Amazonia. Kwa kukabiliana kwa dhati kabisa na uhaba mkubwa wa mihimili ya uinjilishaji wa kina, hali inayowafanya waamini wa Amazonia kukosa huduma makini na endelevu za kichungaji, kiasi hata cha kujisikia kwamba, wametelekezwa na Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.