2018-04-12 06:58:00

SECAM na CCEE yanajadiliana kuhusu changamoto za utandawazi!


Utandawazi umekuwa na athari kubwa sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kuna makundi ya watu wanaendelea kufaidika kutokana na mchakato wa utandawazi, lakini, waathirika wakubwa ni vijana! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni matokeo ya utandawazi, athari za mabadiliko ya tabianchi na mtikisiko wa uchumi, kitaifa na kimataifa. Mambo yote haya yanayoacha ukakasi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwani kama walivyosema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican: uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi hasa za wale maskini na wale wanaoteseka ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia!

Kanisa linapenda kusoma alama za nyakati na kuzifafanua mintarafu mwanga wa Injili, ili kujibu changamoto hizi na kuzipatia maana mpya kadiri ya tunu msingi za Kiinjili. Hizi ndizo changamoto ambazo zinavaliwa njuga na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE katika mkutano wa ushirikiano baina ya Mabaraza haya mawili kuanzia tarehe 12-15 Aprili 2018, huko Fatima, nchini Ureno. Mkutano huu unafanyika kwa faragha kwa kuwahusisha viongozi wakuu wa Mashirikisho ya Mabaraza haya mawili.

Athari za utandawazi katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ughaibuni; utu na heshima ya binadamu sanjari na ekolojia ya mazingira, kama sehemu ya utunzaji wa kazi ya uumbaji ni kati ya mada zinazochambuliwa na Mababa hawa wa Kanisa huko Fatima, Ureno. Monsinyo Duarte Nuno Queiroz de Barros da Cunha, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE katika mahojiano maalum na Vatican News, anasema, tangu mwaka 2004 kumekuwepo na ushirikiano wa karibu sana kati ya SECAM na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya.

Lengo kuu limekuwa ni kwa Maaskofu kushirikishana, uzoefu, mang’amuzi na changamoto ambazo kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wanaweza kuzifanyia kazi kwa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Katika mkutano huu, SECAM inawakilishwa na Askofu mkuu Gabriel Mbilinyi, Rais wa SECAM. Kutokana na ushirikiano na mshikamano huu, Mabaraza haya yamekuwa mstari wa mbele kujibu changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa ufanisi mkubwa zaidi. Kwa mwaka huu, dhana ya utandawazi na athari zake, ndiyo inayofanyiwa kazi na Maaskofu kutoka SECAM na Bara la Ulaya kwani madhara yake ni makubwa katika ustawi, maendeleo, mafao na mafungamano ya kijamii.

Utandawazi, umewezesha watu kutoka katika mataifa mbali mbali kukutana, kushirikiana na kushikamana, lakini bado kuna changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi hasa katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kujikita katika malezi ya awali na endelevu, ili kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari utakaoyawezesha Makanisa mahalia kusaidiana, kushikamana na kukamilishana. Utandawazi, usipoangaliwa kwa jicho la pekee, unaweza kuharibu mila, desturi na maisha ya watu wengi hasa Barani Afrika kwa kutaka kuiga mitindo ya maisha isiyokuwa na mvuto wala mashiko kwa utu na heshima ya binadamu.

Dhana ya ndoa za watu wa jinsia moja, malezi na makuzi ya watoto, matumizi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, uhuru usiokuwa na mipaka ni kati ya changamoto zinazohitaji kuvaliwa njuga na Mababa wa Kanisa, ili kweli mchakato wa utandawazi uweze kuwa na mafao makubwa zaidi, kuliko kuhatarisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Kuna sera na mikakati inayotaka kuhalalisha utamaduni wa kifo na mambo yanayosigana na Injili ya familia. Uchu wa mali na madaraka ni changamoto pevu kwa viongozi wengi na matokeo yake ni kinzan, ghasia na majanga kwa watu wasiokuwa na hatia. Mkutano huu, umefadhiliwa na Kardinali Manuel Clemete, Patriaki wa Lisbon, Ureno, anayetaka wajumbe hawa kupata ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.