2018-04-12 10:12:00

Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa yaliyotokea Algeria!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa ya ajali ya ndege ya kijeshi iliyoanguka, Jumatano, tarehe 11 Aprili 2018 na kusababisha zaidi ya watu 257 kupoteza maisha yao papo hapo! Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Paul Desfarges, wa Jimbo kuu la Algeri, nchini Algeria anasema, anapenda kuungana na ndugu, jamaa na familia ya Mungu nchini Algeria kuomboleza msiba huu mkubwa.

Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma, upendo na msamaha kuwapokea marehemu wote waliofariki katika ajali hii katika mwanga na amani ya milele. Anawaombea majeruhi waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli zao za kawaida. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaombea wale wote wanaoendelea kutoa msaada kwa waathirika wa janga hili faraja ya Mwenyezi Mungu, iweze pia kuwafikia wananchi wote wa Algeria! Habari zaidi zinasema, Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Algeria, Ahmed Gaid Salah ameunda Tume itakayofanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hii kubwa kuwahi kutokea nchini Algeria katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni! Serikali ya Algeria imetangaza siku tatu za maombolezo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.