2018-04-12 16:28:00

Bi Lagarde ameingilia kati ya mzozo wa kibiashara kati China na Marekani!


Masoko makubwa ya hisa ya barani Ulaya yametetereka baada ya Mkurugenzi  wa Shirika la Fedha Kimataifa,(IMF) Bi  Christine Lagarde, kutoa tahadhari juu ya vita vya kibiashara. Bi  Christine Lagarde ameingilia  kati katika mzozo wa kibiashara baina ya Marekani na China na kutoa tahadhari kwamba, vizingiti vya kibiashara vitahujumu ustawi wa uchumi wa Dunia.  Akihutubia kwenye kongamano huko Hong Kong nchini China, Mkurugenzi huyo wa shirika la fedha kimataifa aidha amesema, ustawi wa uchumi wa dunia unaimarika lakini wakati huo huo ametahadharisha juu ya vita vya kibiashara.

Masoko ya hisa ya London, Frankfurt na  Paris yalipanda na kushuka yakiwepo matumaini kwamba vita vya kibiashara baina ya Marekani na China vitaepushwa. Hata hivyo Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, ni kosa kuzingatia nakisi za biashara kuwa ni ishara ya biashara isiyokuwa ya haki kama ambavyo rais Trump amekuwa anadai mara kwa mara kama jinsi inavyoshuhudiwa sasa katika mzozo na China.

Kutokana na mivutano kati ya nchi ya China na Marekani kuhusu masuala ya biashara, Bi Lagarde amesema, nchi zinapaswa kuweka biashara zao wazi zaidi, kwa kufanya mageuzi ya ndani badala ya kuweka vizingiti. Amesisitiza kuwa serikali zinapaswa kuendesha sera za kujiweka mbali na vita vya kibiashara. Ametahadharisha kwamba, mfumo wa sheria na ulio na wajibu sasa umo katika hatari ya kusambaratika!
 
Sr Angela Rwezaula 
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.